In Summary

•Bw Anthony Adera aliaga dunia takriban wiki mbili zilizopita na mipango ya mazishi yake bado inaendelea.

•Stivo alimfahamisha marehemu jinsi mama yake alivyojawa na mawazo na maumivu moyoni kufuatia kifo chake.

Mwanamuziki Stivo Simple Boy
Image: HISANI

Mwimbaji Stephen Otieno Adera almaarufu Stivo Simple Boy ameendelea kumuomboleza marehemu baba yake wiki mbili baada ya kuaga dunia.

Bw Anthony Adera aliaga dunia takriban wiki mbili zilizopita na mipango ya mazishi yake bado inaendelea.

Huku akiendelea kumuomboleza mzazi huyo wake, Simple Boy amemuandikia barua akimueleza jinsi moyo wake unaumia kwa kumpoteza.

Katika shairi lake la mistari 16, rapa huyo kutoka Kibra alidokeza ahadi nyingi za maisha mazuri ambazo alikuwa amempa marehemu baba yake.

Mwimbaji huyo pia alimfahamisha marehemu baba yake jinsi mama yake alivyojawa na mawazo na maumivu moyoni kufuatia kifo chake.

Soma shairi ya Stivo hapa;

"Hello baba naindika barua

Siku imefika ujaiona hata jua

Moyo yaniuma kaburi NATUPUA UA

Rest in peace MI nakuombea dua

Nlikuhahidi majumba nazo magari

Ila umeenda hata bila nusu shari

Mambo dunia yanatia wasiwasi

Oooh my God naisema wazi

Hii maisha uwezi tabiri ya kesho

Yote yanapita duniani kama pepo

Mama anawaza ila namtia nguvu

Namkumbatia Kisha nampiga busu

Roho yaniuma Nashindwa nahema

Nabaki nawaza ndo sitakuona tena

Umeondoka mapema ila safari iwe njema

Ingekuwa uwezo wangu baba si ungerudi Tena"

Wiki mbili zilizopita, rapa huyo alidokeza kuwa inauma sana kumpoteza mzazi huyo wake na kuwaomba mashabiki kuendelea kusimama naye.

"Ningependa kuwaambia mashabiki wangu kwamba nimepata msiba ya kupoteza babangu mzazi Anthony Adera. Ni uchungu sana kupoteza mzazi ila naomba mniombee na mnisapoti kwa huu wakati mgumu," alisema.

Stivo aliwataka mashabiki wake kumuombea na kumpa nguvu huku akiendelea kumuomboleza baba yake mpendwa.

Hafla ya kuchangisha pesa za mazishi ya marehemu Antony Adera imeratibiwa kufanyika hivi leo, Februari 5, katika kanisa la Kibera Lindi Catholic kuanzia mwendo wa saa nane alasiri. Wakenya pia wameombwa kuchanga kupitia Paybill 8280220 ikifuatiwa na jina kama nambari ya akaunti.

View Comments