In Summary

•Nadia amewaomba radhi mashabiki ambao walijitokeza kwenye tamasha lake mjini Kisumu baada ya kulazimika kuondoka jukwaani mapema.

•Mwimbaji huyo aliendelea kuwashukuru mashabiki wote ambao walijitokeza kwenye tamasha hilo.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Malkia wa muziki wa Kenya Nadia Mukami amewaomba radhi mashabiki ambao walikuwa wamejitokeza kwenye Tamasha lake mjini Kisumu siku ya Jumapili baada ya kulazimika kuondoka jukwaani mapema.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alieleza kuwa shoo hiyo ilikatizwa kabla ya kukamilika kutokana na matatizo ya kiafya ambayo yalimkumba akiwa kwenye jukwaa.

Alisema tatizo la pumu ambalo amekuwa nalo kwa muda mrefu lilimfanya ashindwe kupumua alipokuwa akitumbuiza na hivyo akalazimika kukatiza burudani mapema kuliko ilivyokuwa imepangwa.

"Kwa mashabiki wangu wa Kisumu, samahani kutumbuzia kwangu kulikatizwa kwa sababu ya maswala ya kiafya. Nina ugonjwa wa pumu na kabla ya shoo nilikuwa na maumivu ya kifua lakini nilidhani ningeweza kutumbuzia, kwa bahati mbaya katikati ya shoo sikuweza kupumua," Nadia Mukami alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja aliendelea kuwashukuru mashabiki wote ambao walijitokeza kwenye tamasha hilo.

"Nitarejea. Asanteni kwa kunionyesha upendo mkubwa. Shukrani za pekee kwa mapromota kwa sapoti yao. Asante klabu ya Da Place na timu. Pamoja na timu ya ulinzi," alisema.

Nadia Mukami hata hivyo alifichua kwamba kwa sasa afya yake tayari imeimarika na anaendelea vizuri.

Takriban mwaka mmoja uliopita, Nadia alifunguka kuhusu jinsi alivyokejeliwa na kukosolewa sana mitandaoni kwa kukosa kumaliza kutumbuiza katika tamasha yake mjini Busia mwaka wa 2021.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema kwamba alikosa kumaliza shoo hiyo kwa kuwa alilemewa.Alifichua kwamba kwa wakati huo alikuwa anapitia kipindi kigumu baada ya kupoteza mimba mapema wiki hiyo.

"Kuna promoter wa Busia alikuwa amelipa pesa kiasi kitambo. Hapo awali singeweza kutumbuiza kwa sababu ya lockdown. Baada ya lockdown kuondolewa sasa ningeweza kutumbuiza. Nilitoka hospitali siku ya Jumatano alafu akasisitiza lazima nitumbuize Jumamosi hiyo," Nadia alisimulia kwenye mtandao wa Youtube.

Mwanamuziki huyo alidai kwamba waandalizi wa tamasha hiyo walimuweka katika mazingira hafifu na walimtendea vibaya.

Alisema wakati alipoalikwa jukwaani aliweza kutumbuiza kwa nusu saa tu ila akashindwa kuendelea. Alieleza kwamba promota alitaka aendelee kutumbuiza kwa lazima.

"Nilikuwa siwezi kusonga sana kwa kuwa nilikuwa nimetoka hospitalini. Aliita wahuni wake akasema siwezi kutumbuiza kwa dakika 30 nirudi kwenye jukwaa. Kidogo tupigane," Alisimulia.

Mume wake, Arrow Bwoy alisema tukio hilo lilimvunja moyo sana nusura aende kukabiliana na promota huyo.

View Comments