In Summary

•Koffi Olomide amethibitisha ahadi yake ya awali kwa mashabiki wa Kenya kwamba hatatoa chochote isipokuwa shoo ya kusisimua.

•Mawakili walisema Aces & Light Company Limited ndiyo wamiliki wa kipekee wa haki za ‘Koffi Olomide Live – The Peace Concert’ bila uhusiano na wahusika wengine.

Mwanamuziki wa Rhumba wa Kongo Koffi Olomide.
Image: BRIAN SIMIYU

Mwimbaji maarufu wa Rhumba wa Kongo Koffi Olomide amethibitisha ahadi yake ya awali kwa mashabiki wa Kenya kwamba hatatoa chochote isipokuwa shoo ya kusisimua wakati wa tamasha lake la amani Jumamosi hii.

Kupitia kwa mawakili wake, Olomide alipuuzilia mbali vitisho kwamba tamasha hilo litasitishwa kwa madai kwamba anadaiwa pesa na promota mmoja wa humu nchini kwa tamasha lililobatilishwa la 2016.

Tamasha la ‘Koffi Olomide Live – The Peace Concert’ limeandaliwa na Aces & Light Company Limited.

"Mpangaji wa hafla hiyo anasimama kwa uthabiti katika kutupilia mbali madai yasiyo na msingi yaliyotolewa hivi majuzi. Mashtaka yaliyoletwa dhidi ya Koffi Olomide yamekaguliwa kwa kina na kupatikana kuwa ya kipuuzi, ya kuudhi, na yasiyo na maana wala msingi,” Conrad Law Advocates walisema katika taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi jioni.

Ilifuatia madai ya Nsana Productions kwamba Olomide alikiuka masharti ya kimkataba ya tamasha la Machi 2016 ambapo walitaka kurejeshewa pesa pamoja na riba.

Kampuni hiyo ya mawakili, hata hivyo, ilisema Aces & Light Company Limited ndiyo wamiliki wa kipekee wa haki za ‘Koffi Olomide Live – The Peace Concert’ bila uhusiano na wahusika wengine.

"Licha ya majaribio mabaya ya kutatiza tamasha la amani lililotangazwa na watu wengi, tungependa kuthibitisha kwa imani kubwa kwamba tamasha hilo linalotarajiwa sana litaendelea kama ilivyopangwa Jumamosi, Desemba 9, 2023, katika uwanja wa ASK Dome katika Uwanja wa Maonyesho wa Nairobi. Tukio hili linaahidi uzoefu usio na kifani kwa wahudhuriaji wote," Conrad Law Advocates walisema.

Mpangaji wa hafla hiyo, Aces & Light Company Limited, alisema wameendelea kujitolea kudumisha viwango vya juu vya uadilifu na weledi katika shughuli zao zote.

"Tunathamini usaidizi na uaminifu wa walinzi na washirika wetu na tunakuhakikishia kuwa ubora na mafanikio ya hafla zetu hayataathiriwa."

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) siku ya Jumatano muda mfupi baada ya kuwasili Kenya, Koffi Olomide alisema amewa’miss mashabiki wake wa Kenya ambao aliahidi kuwatumbuiza kwa uwezo wake wote wakati wa tamasha hilo la Jumamosi.

"Nina furaha zaidi na siwezi kusubiri kuwa jukwaani na kutumbuiza watu wa Kenya. Nina furaha sana kuwa hapa," nyota huyo wa Loi alisema.

Alitoa shukrani kwa serikali na watu wa Kenya kwa jumla akisema "inahisi vizuri kurejea".

 “Hii pia ni nchi yangu, sehemu ya maisha yangu pia ni Kenya, ningependa kuwaambia mashabiki wangu watetee amani na upendo,” alisema.

Tikiti bado zinauzwa, na mashabiki wanaweza kuzifikia kupitia ticketyetu.com.

Tikiti za awali zinakwenda kwa Sh6,000, watakaonunua getini watalipa Sh7,500 na VIP watalipa Sh25,000.

View Comments