In Summary

•Ally B alitangazwa kufariki katika Hospitali Kuu ya Pwani Jumatano alasiri ambapo alikimbizwa baada ya kulalamika kuhusu maumivu.  

•Ruto aliongoza Wakenya katika kumuomboleza mwimbaji huyo baada ya habari za kifo chake kuenea haraka kote nchini.

Marehemu Ally B
Image: HISANI

Wakenya kutoka tabaka mbalimbali wakiwemo wanasiasa na wasanii wakubwa wameendelea kumuomboleza mwimbaji mkongwe mzaliwa wa Pwani, Ali Khamisi Mwaliguli, almaarufu Ally B ambaye alifariki siku ya Jumatano, Novemba 1.

Ally B ambaye anafahamika sana kwa nyimbo zake maarufu kama vile ‘Maria’ na ‘Bembea’ alitangazwa kufariki katika Hospitali Kuu ya Pwani mjini Mombasa Jumatano alasiri ambapo alikimbizwa baada ya kulalamika kuhusu maumivu.  

Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa alifariki kutokana na shinikizo la damu.

Inaripotiwa kuwa mwanamuziki huyo ambaye tasnia yake ilivuma sana mwanzoni mwa miaka ya 2000 alifika nyumbani akiwa hana raha siku ya Jumatano alasiri na alikimbizwa hospitalini ambapo kwa bahati mbaya alifariki.

Rais William Ruto aliongoza Wakenya katika kumuomboleza mwimbaji huyo mzaliwa wa pwani baada ya habari za kifo chake kuenea haraka kote nchini.

Rais alimtaja kuwa mwanamuziki aliyekuza umoja katika jamii.

"Ninaungana na wanamuziki kuomboleza kifo cha Ally B, mwanamuziki aliyetumia talanta yake kukuza umoja na utangamano katika jamii yetu," Ruto alisema.

Aliongeza "Ali Khamisi Mwaliguli aliandika ujumbe wake wa amani ndani ya mioyo yetu, na tutaubeba daima wimbo huo wa maana. Mungu awape faraja familia yake, marafiki na mashabiki wake waliojitolea."

Wasanii wenzake na watu wengine mashuhuri wakiwemo Akothee, Nyota Ndogo, King Kaka, Lulu Hassan, Masauti, Jua Cali, Mike Sonko, Daddy Owen pia waliungana na Wakenya kuomboleza kifo chake.

Daddy Owen alimtaja marehemu kama gwiji katika tasnia ya muziki na kumtambua kwa juhudi zake za kupigania haki za wasanii.

“R.I.P Ally B.. legendari halisi katika anga ya muziki ya Kenya hasa anayewakilisha ukanda wa pwani na kupigania haki za wabunifu kutoka kanda hiyo pia..! Mioyo yangu inaenda kwa familia wakati huu wa huzuni, pole sana kwa msiba wako mkubwa,” Owen aliandika.

Akothee kwa upande wake alishiriki picha zake za kumbukumbu na marehemu na kumtambua kwa jukumu kubwa alilocheza katika kazi yake ya muziki.

"Najua sikukujulia hali kwa muda, lakini pia nimekuwa nikijaribu kusawazisha maisha rafiki yangu 🙏. Kuondoka kwako kumehuzunisha moyo wangu. 💔, Safari tulizofanya Ulaya zilinifanya kuelewa unyenyekevu ni nini. Lala Salama Bro,” alisema.

View Comments