In Summary

•DJ Fatxo amekuwa kimya sana katika muda wa miezi miwili iliyopita baada ya kuhusishwa na kifo cha Jeff Mwathi.

•Fatxo aliandika ujumbe wa kutia motisha ambao ulionekana kuhusishwa na yale ambayo amepitia katika miezi miwili iliyopita.

Image: FACEBOOK// DJ FATXO

Mwanamuziki mashuhuri wa Mugithi na mcheza santuri Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo anaonekana kujaribu kurejea kwenye tasnia ya burudani siku chache baada ya madai ya mauaji ya Jeff Mwathi kuondolewa kutoka kwake.

DJ Fatxo amekuwa kimya sana katika muda wa miezi miwili iliyopita baada ya kuhusishwa na kifo cha kijana huyo wa miaka 23.Hata hivyo, angu kuondolewa tuhuma za mauaji mapema wiki hii, amekuwa akiwahutubia mashabiki wake.

Siku ya Alhamisi, aliandika ujumbe wa kutia motisha ambao ulionekana kuhusishwa na yale ambayo amepitia katika miezi miwili iliyopita. Mwimbaji huyo wa Kikuyu alidokeza kwamba amepitia wakati mgumu uliomvunja.

"Watu jasiri pia husononeka. Wanapambana tu kwa faragha na kujijenga upya kimya kimya. #djfatxo #mwanawamutumia," DJ Fatxo alisema kwenye Facebook na kuambatanisha na picha yake akiwa ameshika kinanda.

Pia alibadilisha picha yake ya wasifu kwenye mtandao huo wa kijamii, akidokeza zaidi kuhusu kurejea kwake.

DJ Fatxo alivunja ukimya wake wa muda mrefu Jumatano baada ya DPP kumwondolea tuhuma za kuhusika katika kifo cha kutatanisha cha Jeff Mwathi.

Mwimbaji huyo alifungua taarifa yake kwa kutoa pole kwa familia ya marehemu Jeff, marafiki na wote walioguswa na hali hiyo.

"Natumai nyote mnaendelea vyema. Nilitaka kushughulikia madai ya hivi majuzi ambayo yamekuwa yakienezwa kunihusu na kuhusika kwangu katika kifo cha rafiki yangu Jeff Mwathi. Kwanza kabisa, ninataka kueleza huruma zangu za dhati kwa familia na marafiki wa Jeff, na kwa mtu mwingine yeyote ambaye ameathiriwa na hali hii.

Ninajua kuwa huu umekuwa wakati mgumu kwa watu wengi, na ninataka kukiri uchungu ambao umesababishwa na shutuma hizi,” Fatxo alisema kwa sehemu.

Aliendelea kueleza umma kuwa hajapatikana na hatia ya mauaji ya Jeff Mwathi na maafisa wa upelelezi wa DCI na ODPP.

“Pia nataka kuchukua fursa hii kusafisha jina langu na kuwahakikishia nyote kwamba nimepatikana sina hatia baada ya uchunguzi wa kina wa maafisa wa upelelezi wa DCI na ODPP.

"Ingawa nimefarijika kuwa haya nyuma yangu, najua kwamba bado kuna watu ambao wanaweza kuwa na shida na hisia za hasira, kufadhaika, na kukatishwa tamaa," aliongeza.

DJ Fatxo zaidi aliwaonya wanamitandao dhidi ya kukurupuka na kudhulumu wengine kwenye mtandao kila jambo lolote linapotokea.

“Ninataka kutumia hali hii kutukumbusha sote umuhimu wa kutokurupuka kufikia hitimisho au uonevu wa mtandaoni kwa mtu yeyote kwa msingi wa shutuma au hadithi za tetesi. Kama wengi wenu mnavyojua, nimepitia kipindi kigumu sana kihisia na kimwili, na ninajua moja kwa moja jinsi inavyoweza kudhuru na kuumiza kuwa mtu wa kupokea shutuma za uwongo na uonevu mtandaoni,” aliongeza.

Kwa kumalizia DJ Fatxo alisema; “Wacha sote tuchukue muda kutafakari jinsi tunavyoweza kuwa na huruma zaidi, kuelewana na kuheshimiana. Ninaelewa kuwa hali hii inaweza kuwa ngumu kwa baadhi yenu, na ninataka kuhimiza kila mtu kutafuta ukweli na kukabiliana na hali hii kwa nia iliyo wazi na moyo wa huruma.

"Tutumie hali hii kama fursa ya kujumuika pamoja, kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu, na kukua kama mtu mmoja mmoja na kama jamii. Asanteni sana kwa sapoti inayoendelea na kuelewa kwenu wakati huu mgumu. Ninawashukuru kila mmoja wenu, na ninatumai kwamba sote tunaweza kusonga mbele kwa neema na upendo."

View Comments