Mtangazaji mmoja wa televisheni aliyeshukiwa kumshambulia mwanaume mmoja na kusababisha kifo chake anachunguzwa.

Antony Nyongesa Namasaka wa televisheni ya Nyota alifikishwa mbele ya mahakama moja huko Madaraka pamoja na mhusika wenzake Kennedy Muyale kwa kusababisha kifo baada ya vita kwenye klabu.

Lawrence Okoth aliaga dunia huku akipokea matibabu katika hospitali kuu ya Kenyatta.

Polisi waliomba kuwaweka korokoroni, siku kumi na nne,  washukiwa hawa huku uchunguzi ukiendelea. Komanda wa polisi Peter Kamau aliiambia mahakama kuwa kisa hicho kilitokea katika klabu ya Dallas, Umoja, tarehe kumi na sita mwezi wa Mei ambapo Okoth alikuwa anajiburudisha kwa vinywaji.

Aliaga dunia siku iliyofuata.

''MWENDAZAKE ALIKUFA HOSPITALINI AkIPOKEA MATIBABU NA BAADA YA UPELELEZI MAJIBU YALIONYESHA KUWA ALIAGA KUTOKA KWA MAJERAHA YA CHOMBO BUTU. NAHITAJI WAKATI ZAIDI KUREKODI KAULI YA WATEJA AMBAO WALIKUWA KATIKA KLABU SIKU AMBAYO MWENDAZAKE ALICHAPWA,''KAMAU ALIIAMBIA MAHAKAMA.

Washukiwa walikamatwa tarehe thelathini na moja mwezi wa Mei baada ya tukio kuripotiwa Mei tarehe ishirini na moja.

Ombi hilo lilikataliwa na washukiwa ambao walikiri kuwa wameajiriwa kazi ya kudumu hivyo ikiwa watawekwa kizuizini waweza kupoteza kazi zao.

Namasaka aliiambia mahakama kuwa yeye ni mtangazaji wa televisheni ya Nyota na familia yake ilitegemea mapato ya kazi yake kujikimu.

Muyale pia aliomba aachiliwe kwa dhamana huku akisema kuwa alifanya kazi na Air Kenya katika idara ya oparesheni.

Wote waliomba waachiliwe kwa dhamana huku wakisema kuwa ni watu halisi na kuwa wangeenda mbele ya afisa anayesimamia uchunguzi wakati wowote wangehitajika.

Mashtaka hata hivyo ilishikilia kuwa watawekwa rumande kwa kuwa hakuna vifaa vilivyo onyeshwa kwenye mahakama kuthibitisha kuwa ni wafanyakazi wa kampuni hizo na madai kuwahusu ni mazito''.

Hakimu mkuu alitoa uamuzi kuwa kikatiba, wanahaki ya kupewa dhamana na kuskia ombi kuwa wangepoteza kazi zao ikiwa wangewekwa korokoroni.

''NAWAPA DHAMANA YA SHILINGI ELFU MIA TATU NYOTE AU ELFU MIA MOJA KILA MMOJA,''ALISEMA

Aliagiza kila mshukiwa alete vitambulisho vyao vya kazi mbele ya mahakama kabla ya kuachwa huru na kuwa lazma wangejitokeza mbele ya afisa wa upelelezi wakati wowote wangehitajika.

Kesi hiyo itatajwa Juni tarehe kumi na saba.

View Comments