Mwili wa mwanaume mmoja aliejirusha kwenye mto Sio karibu na soko la Matayos wikendi iliopita umepatikana.

Mwili huo umepatikana leo asubuhi na wapiga mbizi ambao wamekuwa wakikesha kwenye mto huo wakiutafuta.

Wapiga mbizi hao wameomba serikali kuingilia kati na kuwapa vifaa vya kisasa vya kutafuta miili.

Kwingineko sare za shule za wanafunzi wawili wa shule ya msingi ya Nambale AC waliotoweka juma moja lililopita zimepatikana kichakani kilomita mbili kutoka shuleni humo.

Mzazi wa watoto hao anasema walienda shuleni wakihofia kuchapwa na mwalimu baada ya kudaiwa kuiba vitabu vya wenzao.

Kando na hayo, chama cha kutetea maslahi ya walimu KNUT tawi la Taita Taveta kimeonya kuwa huenda mtaala mpya wa elimu ukakosa kutekelezwa kikamilifu iwapo wizara ya elimu haitahusisha wadau wote.

Katibu wa chama hicho Lenox Mshila anasema shurutisho la kufunza mtaala huo mpya kilazima huenda zikaathiri pakubwa kiwango cha elimu nchini na kushauri wadau wote kujadiliana kwa kina na kuafikiana kuhusiana na mtaala huo kwa lengo la kufanikisha elimu.
View Comments