Kanze Dena

Rais Uhuru Kenyatta amefaulu kuafikia makubaliano na benki kuhusu mbinu bora za kuwapa vijana mikopo nafuu, almaarufu Stawi. Kufuatia msururu wa mashauriano na Rais, benki sasa zitaanza kutoa mikopo kwa riba ya asilimia 9 kwa vijana ili kuwasaidia kuanzisha shughuli za kujipa mapato.

Rais Kenyatta pia alibainisha wazi kwamba kabla ya kuafikia makubaliano hayo, benki zilielezea wasiwasi kuhusu uwezo wa baadhi ya vijana kulipa mikopo wanayopewa. Akiarifu waandishi wa habari, Msemaji wa Ikulu Kanze Dena-Mararo hata hivyo alisema vijana wengi wanaofanya biashara wanalipa vyema mikopo waliopewa na hivyo kupunguza riba kutawamotisha zaidi.

Akihutubia taifa kwenye sherehe za kuadhimisha Siku Kuu ya Madaraka katika Kaunti ya Narok, Rais Kenyatta alisema Serikali yake inatekeleza hatua kadhaa kukabiliana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Tangu mwaka uliopita, Rais amekuwa akishughulikia mpango huo wa ajira ambao utazinduliwa Alhamisi wiki hii. Juhudi hizi za pamoja kati ya Serikali na Wakfu wa Masterdard zinatokana na mashauriano yaliyofanyika pembezoni mwa Kikao Kikuu cha Umoja wa Mataifa mwaka uliopita. Msemaji wa Ikulu pia alisema Rais Kenyatta yuko makini kuhakikisha sehemu zote za nchi hii zinanufaika na miradi mbali mbali inayotekelezwa na Serikali yake.

Aidha, alisema Kiongozi wa Taifa amekuwa katika mstari wa mbele kutetea haki na uwakilishi wa wanawake katika nyadhifa za uongozi. Wakati wa Kongamano la Wanawake la mwaka huu lililofanyika juzi Nchini Canada, Rais alipongezwa kutokana na juhudi zake za kutetea ajenda ya usawa wa kijinsia Barani Afrika.

View Comments