Kizungu Mkuti:Wabunge wanafaa kuwa mawaziri?
Wabunge wamekuwa wakishinikiza kurekebishwa kwa sheria ilia kumwezesha rais kuwateua wabunge kuwa mawaziri . Katiba mpya iliyopitishwa na wakenya iliwazuia wabunge kuteuliwa kuwa mawaziri lakini sasa pendekezo hilo limeanza kuungwa mkono . Aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura ni wa hivi punde kuunga mkono pendekezo hilo akisema kutowatumia wabunge kama mawaziri wa serikali ni jambo ambalo limezua uhasama kati ya viongozi wa kisiasa na wale wa utawala wa serikali .
Dhamira kubwa ya kuwateua watalaam kuhudumu kama mawaziri ilikuwa kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao kikamilifu bila muingilio wa kisiasa lakini hilo limekosa kuzaa matunda kwani utendakazi wa mawaziri watalaam haujaweza kuisadia serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi . Wadadisi pia wanaamini kwamba hatua kuwanyima wabunge fursa ya kuwa mawaziri ndio hatua inayofaa kulaumiwa kwa hamu yao ya kutaka kuongezwa mishahara na kujiongeza marupurupu kila mara.
Wanaounga mkono hatua ya kuwateua wabunge kuwa mawaziri wamesema hatua hiyo itaiwezesha serikali kuokoa fedha kwani haitawalipa mawaziri na wabunge ila mbunge anayeteuliwa kuwa waziri ataongezwa takriban shilingi laki nne kwa mshahara wake wa sasa kama mjumbe .Pia wanasema pesa zinazotumiwa kuwalipa wafanyikazi wa mawaziri wa sasa ,magari na marupurupu zitaweza kuokolewa endapo wabunge wataweza kuteuliwa kuwa mawaziri . Je unaunga mkono pendekezo la kuwateua wabunge kuwa mawaziri?