OPARANYA

Kesi iliyowasilishwa na magavana katika mahakama ya upeo kutaka ufafanuzi kuhusu sheria ya ugavi wa pesa katika kaunti itatajwa siku ya Ijumaa wiki hii.

Baraza la magavana liliwasilisha kesi kupinga hatua ya serikali na bunge la kitaifa kupunguza mgao wa fedha za kaunti.

Mwenyekiti Wycliffe Oparanya alisema kwa sasa shughuli za kaunti zote 47 zimesitishwa kutokana na kutokuwepo kwa fedha. Alisema kulingana na ratiba ya matumizi ya pesa za serikali wangekuwa tayari washapokea fedha lakini kwa sababu ya utata uliyopo hakuna pesa zilizotumwa kwa kaunti.

Alisema ni vigumu kwa serikali za kaunti kutengeneza bajeti na ilhali magavana hawajui ni pesa ngapi watapokea kutoka kwa hazina kuu.

Oparanya Jumatatu asubuhi aliongoza magavana na mamia ya wakilishi wadi kuandamana nje ya mahakama ya upeo wakilalamikia hatua ya serikali ya kitaifa na bunge la kitaifa kupunguza mgao wa pesa za kaunti.

Oparanya alisema baraza la magavana lilikuwa limependekeza mgao wa shilingi bilioni 344 nayo wizara ya fedha ikipendekeza bilioni 310.

Anasema baada ya vuta ni kuvute na kwa ushirikiano wa mdhabibiti wa bajeti waliafikiana shilingi bilioni 325.

Hata hivyo walitamaushwa na hatua ya bunge la kitaifa kudinda kuidhinisha kiwango cha fedha kilichokuwa kimeidhinishwa na seneti na kupunguza pesa hizo hadi bilioni 316.

Hatua hii ilizua mtafaruku na kukwamisha zoezi la kupitisha mgao wa fedha za kaunti ili shughuli za kaunti ziendelee kama ilivyokuwa imepangwa. Magavana hao walifika katika mahakama ya Juu kutaka ufafanuzi kuhusu sheria ya ugavi wa raslimali za serikali.

Miongoni mwa magavana waliokuwepo wakati wa kuwasilishwa kwa kesi hiyo ni Mwenyekiti wa baraza na magavana ambaye pia ni gavana wa Kakamega Wycliffe Opranya, James Ongwaye wa Kisii, Ali Roba wa Mandera, Martin Wambora wa Embu, Jefferson Kingi wa Kilifi, Wilbur Otichilo  na Anyang Nyong’o wa Kisumu.

View Comments