mradi wa kawi

Rais Uhuru Kenyatta hapo jana alizindua mradi wa Ziwa Turkana unaozalisha kawi kutokana na upepo na ambao ndiyo mkubwa zaidi barani Afrika.

Mradi huo una uwezo wa kutoa megawati 310 za nguvu za umeme safi, za kutegemeka na pia wa gharama nafuu.

Wakati huo huo Rais Kenyatta alizindua laini ya nyaya za kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 428 na vile vile akazindua mradi wa kuboresha barabara kutoka Loiyangalani hadi South Horr.

Laini hiyo yenye uwezo wa megawati 1,200 iliyojengwa na kampuni ya usafirishaji wa umeme ya KETRACO unatoa stima inayozalishwa katika mradi huo hadi Suswa ambako inaingizwa katika mtandao wa kitaifa.

Katika miezi minane iliyopita, mradi huo wa nguvu za umeme umepunguza matumizi ya stima yenye thamani ya zaidi ya shilingi 8 kwa kupunguza matumizi ya kawi inayotokana na mashini zinazotumia mafuta ya petroli. Katika kipindi hicho hicho, mradi huo ulitoa nguvu za umeme za kilowati milioni 1.2.

Rais Kenyatta, akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto, alisema kuzinduliwa kwa mradi huo ni fahari kuu kwa Kenya.

“Kwa kuafikia jambo hili kuu, huku Kenya ikivunja rekodi barani Afrika, natoa changamoto kwa Wakenya wote waendelee kuwa wajenzi wajasiri wanaofanya kazi vyema zaidi wanapotakiwa kutenda jambo kuu,” kasema Rais Kemnyatta.

Kenya ni mojawapo ya mataifa ytanayoongoza ulimwenguni katika ustawi wa kawi mbadala hasa katika sekta inayotengeneza kawi kutokana na mvuke.

Rais ambaye alifanya matembezi katika mradi huo alisema serikali imeongeza juhudi za kustawisha miradi ya kukuza kawi kutokana na upepo na vyanzo vingine vya kawi mbadala na safi inayotekelezwa na Shirika la KenGen na sekta ya kibinafsi.

Uwezo wa Kenya wa kawi iliyostawishwa umeongezeka kutoka Megawati 1,738 katika mwaka wa 2013 hadi kiwango cha sasa cha Megawati 2,713 huku mradi wa Kawi wa Ziwa Turkana, Mradi wa kawi kutokana na jua wa Garissa (54 MW) na mradi wa Kawi kutokana na upepo wa Ngong (26 MW) ikiingia katika mtandao wa kawi wa kitaifa katika mwaka mmoja uliopita.

Rais Kenyatta alisema kuzinduliwa kwa mradi huo ni dhihirisho la kujitolea kwa Kenya kuimarisha vyanzo vya kawi safi na isiyo na madhara kwa mazingira. Pia inaimarisha ahadi ya Kenya katika nyanja za kimataifa ya kupunguza athari za gesi hatari kwa mazingira.

Alisema Kenya inasherehekewa kuwa mojawapo ya mataifa yanayoongoza ulimwenguni kwa matumizi ya kawi ya hadi aslimia 85 kutokana na vyanzo safi na visivyodhuru mazingira hasa kawi kutokana na mvuke na kwa kutumia teknolojia ambayo imefanya Kenya kuwa kituo cha ufanisi mkubwa barani Afrika.

“Utekelezaji uliofana wa mradi wa kawi kutokana na upepo wa Ziwa Turkana unadhibitisha sifa za Kenya kuwa kituo bora cha uwekezaji barani Afrika na mfano mwema wa fursa kubwa ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” kasema Rais.

Rais alisema kustawishwa kwa kawi safi nchini Kenya kutahakikisha urembo wa mandhari yake na mazingira bora yamehifadhiwa na kulindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Alisema kukamilika kwa mradi huo na kuanzishwa kwa shughuli zake ni dhihirisho la jukumu kubwa inayotekelezwa na ushirikiano kati ya sekta za umma na kibinafsi katika ustawi wa nchi hii.

“Nawakaribisha waekezaji, sio tu kwa sekta ya kawi lakini pia katika nyanja zote za uchumi, kuungana na serikali kubuni na kutekeleza miradi yenye kuleta mabadiliko yanayoleta faida kwa watu wetu na pia waekezaji,” kasema Rais.

Naibu wa Rais Ruto alisema ufanisi wa mradi huo unatokana na umoja na kujitolea kwa washika dau wote wakiwemo jamii ya eneo hilo, wafadhili wa maendeleo na sekta ya kibinafsi.

Dkt Ruto alimshukuru Rais kwa binafsi kusimamia mradi huo, ambao una mitambo 365 ambayo kila mmoja unazalisha megawati 850 za umeme, na kuhakikisha umetekelezwa kwa ufanisi.

Waziri wa Kawi Charles Keter alisema wizara yake inahakikisha wenyeji wa sehemu hiyo wameunganishwa na mtandao wa umeme wa kitaifa haraka iwezekanavyo. Mwenyekiti wa mradi huo Mugo Kibati alisema mradi huu ulio chini ya Ruwaza ya Maendeleo kufikia mwaka wa 2030 unadhibitisha kukomaa kwa Kenya kuwa kituo kipendwacho cha uekezaji barani Afrika.

Wengine waliozungumza ni Gavana wa Marsabit Mohamud Ali na mwenzake wa Samburu Moses Lenolkulal. Viongozi hao wawili walimpongeza Rais Kenyatta kwa kujitolea kwake kuboresha maisha ya wakenya wote kwa kutekeleza miradi ya maendeleo inayoleta mabadiliko kote nchini.

-PSCU

View Comments