cs

Waziri wa elimu Profesa George Magoha ametoa amri kuwa shule ya msingi ya St Catherine Bombolulu katika eneo bunge la Kibra ifungwe kutokana na miundo msingi duni.

Magoha alisema shule hiyo ilikuwa na miundo msingi hatari sawia na ile ya shule ya Precious Talent ambapo madarasa yaliporomoka na kusababisha vifo vya wanafunzi saba na wengine wengi kujeruhiwa.

Magoha alizungumza siku ya jumatano wakati alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa shule katika eneo la Kibra.

Magoha alisema kulingana na matokeo, jengo la shule hiyo halikuwa limeidhinishwa na wataalam wa ujenzi.

Waziri pia alikosoa usimamizi wa shule hiyo kwa kuajiri walimu ambao hawajasajiliwa na tume ya kuajiri walimu nchini - TSC.

Magoha alifunga shule ya msingi ya Precious Talent eneo la Dagoreti hadi Jumatatu wiki ijayo pale ripoti kamili ya ukaguzi wa shule hiyo itakapokuwa imekamilika. Amri wa Magoha ilijiri saa chache kabla ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko kutimua maafisa 16 wa kaunti hiyo kwa madai ya utepetevu kazini na kupelekea kutokea kwa mkasa huo.