wairimu

Sarah Wairimu ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya Tob Cohen amekana mashtaka hayo katika mahakama kuu mbele ya Jaji Stella Mutuku, huku wakili Philip Murgor akiruhusiwa kumwakilisha mteja wake mahakamani.

Inadaiwa kuwa kati ya Julai 19 na 20  Sarah Wairimu alimuua Cohen.

Katika kesi hiyo, mwendesha mashtaka Catherine Mwaniki amesema wanahitaji muda zaidi wa kuratibu mipango ya ulinzi kwa mashahidi.

Aidha mahakama hiyo imemruhusu wakili  Murgor kuendelea kumwakilisha mjane Sarah Wairimu.

Jaji Stella Mutuku alisema ni wazi kuwa kuchaguliwa kwa Murgor awali kuwa mwendesha mashtaka wa umma hakungezuia kumwakilisha mteja wake.

Juma lililopita, wakili wa familia ya Cohen, Cliff Ombeta alipinga Murgor kuwakilisha kesi ya Wairimu akidai kwamba

yeye angali mwendesha mashtaka wa umma kwani ilani ya gazeti rasmi haikuwa imetolewa hata baada ya yeye kujiuzulu.

"Hakuna ubishi kwamba alijiuzulu. Ameshughulikia maswala mengine mahakamani," Mutuku alisema.

Mutuku ameongeza kusema kuwa Murgor amejumuika na DPP katika maswala mengine na hawajawahi kuibua maswala yoyote.

"Hakuna mtu anayelazimishwa kubakia afisini. Uchapishaji wa ilani ya gazeti rasmi unanuia kuwajulisha umma na huchapishwa wakati unapojiuzulu, Murgor yuko halali kumwakilisha mteja wake mbele ya korti hii." Alisema.

Mwendesha mashtaka Catherine Mwaniki anasema wanahitaji wakati wa kuwasiliana na mpango wa ulinzi wa mashahidi.

"Hatutaki kuwafichua mashahidi katika hatua hii. Tutatumia baadhi ya taarifa zao ili kutoa kauli zao zinazo tulazimu kuchukua hatua hii," alisema.

View Comments