Safaricom yakana madai ya udukuzi huku ikiomba walionufaika na data, muda wa maongezi kurejesha
Kulikuwa na sintofahamu Jumatano baada ya madai kuibuka kwamba mitambo ya safaricom ilidukuliwa na mtu asiyejulikana na kuruhusu wateja kunufaika na data pamoja na muda wa maongezi wa bwerere inayogharimu mamilioni ya pesa.
Ripoti ambazo hazikuthibitishwa zilisema kwamba mdukuzi huyo alidukua mfumo wa mitambo ya Safaricom na kuwaruhusu wateja kunufaika na idadi ya kubwa ya data bila malipo.
Inasemekana kampuni hiyo ilipata hasara ya data ya thamani ya kima cha shilingi milioni 500 na muda wa maongezi wenye thamani ya shilingi 1 milioni.
Hata baada ya polisi kusema wamemkamata mhusika, Safaricom ilitupilia mbali madai hayo na kusema ni uvumi tu.
Safaricom inawaomba wale ambao walijipatia data na muda wa maongezi bila malipo na kinyume cha sheria kufika katika maduka yao ya karibu ili kurekebisha makosa hayo.
Kamishna wa kaunti ya Kiambu Wilson Wanyanga alisema maafisa wamemkamata mtuhumiwa huyo huko Juja na jamaa huyo atafikishwa mahakamani Alhamisi. Aliwaambia waandishi wa habari mtuhumiwa huyo alikamatwa na kadi za safaricom 1,000 za Simu.
Wanyanga alisema mtuhumiwa huyo, anaamika kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu, alidukua mfumo wa mtambo wa Safaricom na kuruhusu wateja kupata bidha hizo muhimu ambazo huwa ndiyo pato kubwa sana kwa kampuni hiyo.
Safaricom, hata hivyo, walikanusha kuwa hawakujua madai hayo. Meneja wa mawasiliano ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi alisema kwamba polisi walikuwa wamekamata watu wengi ambao wanatekeleza uhalifu wa kubadilisha kadi za simu na kuibia watu pesa kutoka M-Pesa.
"Hatujui kuhusu ya utapeli wa aina hii. Hatuna habari kuhusu kukamatwa kwa mtu yeyote aliyehusika. Tunachojua ni kwamba polisi wamekuwa macho kwa wabadilishanaji haramu wa kadi za simu na na watapeli wa M-Pesa. "alisema.