Watu Watano waaga dunia baada ya gari lao kusombwa na mafuriko Kajiado
Watu watano wa familia moja wameaga dunia leo huko kajiado baada ya gari walimokuwa wakisafiria kusombwa na mafuriko walipokuwa wakivuka daraja la Mto Ng’tataek mapema hivi leo . watano hao walikuwa wakitoka sherehe ya harusi nchini Tanzania kabla ya kumtembelea jamaa yao katika eneo la namanga . kamanda wa polisi kajiado ya kati Daudi ole Lornyokwe amesema baadaye walipokuwa wakielkeea Bissil ili kuvuka daraja hilo,gari lao lilishindwa nguvu na maji na kusombwa
Lornyokwe amesema gari hilo lilikuwa limewabeba mwanamke mmoja na wanawe wawili na wanaume wawili wote wa familia moja . “ Tumeshaiondoa miili yao pamoja na mabaki ya gari hilo ma miili inapelekwa katika hospitali ya rifaa ya Kajiado’ amesema kamanda huyo wa polisi . Kamishna wa kaunti ya Kajiado Joshua Nkatha alikimbia katika eneo la mkasa ili kuzifariji familia za walioathiriwa na maafa hayo .
Mvua kubwa inayozidi kunyesha katika maeneo mengi ya taifa imezidi kusababisha maafa na hasara huku zaidi ya watu 46 wakiaga dunia huko West Pokot baada ya kutokea maporomoko ya ardhi . Idara ya utabiri wa hali ya anga tayari imesema Sehemu nyingi za taifa zitaendelea kupokea kiasi kikubwa cha mvua .idara hiyo imesema maeneo ya kati ,magharibi ,kaskazini mashariki na Rift valley yataathiriwa zaidi .wale wanaoishi katika maeneo ya chini wameshauriwa kuhamia sehemu za juu .Kwingineko wakaazi wa Taita Taveta wametahadharishwa kuhusu uwezekano wa kutokaea maporomoko ya ardhi katika baadhi ya sehemu hiyo kwa ajili ya mvua kubwa inayoshuhudiwa . Maporomoko madogo ya ardhi tayari yameshuhudiwa katika maeneo ya Mbengonyi, Mdangenyi, Msawe na Mbale.