Eto'o

Gwiji wa soka na raia wa Cameroon Samuel Eto'o  mwenye umri wa miaka 38  alitangaza kustaafu kwake Septemba, na sasa arejea darasani kujifunza zaidi kwa kile anasema, 'kurudisha mkono kwa jamii'.

Kwa sasa Eto'o ana azma ya kurudisha mkono kwa jamii yake baada ya kutamba ugani kwa kipindi kirefu.

Akihojiwa na shirika la vyombo vya habari vya Ufaransa, Eto'o alisema kuwa anatazamia kuinua maisha ya watu wasiobahatika katika jamii yake.

"Ningependa kuinua na kuimarisha  maisha ya watu katika bara letu,"  Eto'o alisema.

Eto'o alisema kwamba katika ulingo wa soka, alishughulikiwa ipasavyo na wataalum stadi, na sasa angependa kujifunza mengi ili kuinua jamii pia.

"Ukiwa mwanasoka, unawalipa watu washughulikie taaluma yako na mambo mengi,"

"Lakini ifikapo wakati wako kuwahudumia watu, unafaa kuwa na ujuzi na ili kuwaongoza vizuri, na unahitaji kujifunza mbinu hizo,"

Kwa sasa anatazamia kujiunga na chuo kikuu cha Harvard ili kusomea masuala ya usimamizi wa biashara hapo mwakani.

Katika kipindi cha miaka 20, alishinda zaidi ya tuzo 18 kuu. Miongoni mwa tuzo hizo ni ligi kuu barani ulaya, ambayo alishinda akiwa Barcelona na nyingine akiwa Inter Milan. Pia alishinda Kombe la mataifa barani Afrika  mara mbili pamoja na kunyakua dhahabu katika Olimpiki mnamo 2000.

View Comments