algeria (1)

Algeria leo imetangaza kwamba itaunga mkono Kenya katika juhudi zake za kuwania uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa uchanguzi utakaofanyika mwezi wa Juni mwaka ujao.

Akizungumza alipowasilisha hati zake kwa Rais Uhuru Kenyatta, Balozi huyo mpya wa Algeria hapa nchini Selma Malika Haddadi alisema nchi yake inaamini Kenya ina fursa bora ya kupigania maslahi ya bara la Afrika katika baraza hilo.

“Algeria inaunga mkono Kenya kikamilifu katika kupigania nafasi hiyo. Tunaamini kwamba Kenya ina nafasi bora ya kutetea maslahi ya bara la Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” kasema Balozi Haddadi.

Balozi huyo mpya alisema kujitolea na mchango wa Kenya katika usalama wa kanda na kimataifa kunaifanya Kenya bora zaidi kuwakilisha Afrika katika baraza hilo.

Alisema kuchaguliwa tena kwa Kenya kuwa mwanachama wa Baraza la Muungano wa Afrika kuhusu Amani na Usalama na pia kuidhinishwa kwake na muungano huo  kugombea uanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni dhibitisho kamili kwamba Kenya ni mgombeaji wa msitari wa mbele wa kiti hicho.

Wakati wa hafla hiyo fupi katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta pia alipokea hati kutoka kwa Balozi mpya wa Bangladesh hapa nchini Jahangir Kabir Talukder na pia Balozi Verna Mills wa taifa la visiwa vya Kitts na Nevis ambaye makao yake yatakuwa Jijini Havana, Cuba.

Akipokea hati kutoka kwa mabalozi hao wapya, Rais alisema anatumaini kufanya kazi kwa karibu nao ili kuimarisha uhusiano thabiti kati ya Kenya na nchi zao.

Vile vile, Rais aliwahakikishia kwamba atawuwaunga mkono ili kufanikisha kazi yao hapa nchini.

Balozi Talukder wa Bangladesh alisifu uhusiano wa kirafiki kati ya Kenya na nchi yake na akaahidi kutumia muda wake hapa nchini kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Nairobi na Dhaka.

“Ni matumaini yangu ya dhati kwamba nitafanikiwa katika juhudi zangu za kukuza vyema zaidi uhusiano kati ya Bangladesh na Kenya,” kasema Balozi Talukder.

Kwa upande wake Balozi Mills ambaye ni wa kwanza kuwakilisha taifa la St. Kitts na Nevis hapa Kenya alisema kuwasilisha hati zake kunaashiria mwanzo mpya kati ya nchi yake na eneo la Afrika chini ya Jangwa la Sahara.

“Nikiwa Balozi wa Kwanza wa St. Kitts na Nevis hapa Kenya, ni matumaini yangu kwamba nitafanikiwa kukuza uhusiano ulioko kati ya nchi hizi mbili,” kasema Balozi Mills.

-PSCU

View Comments