nigeria

Wanaume 26 waliovalia kama wanawake wamekamatwa katika sherehe za siku ya kuzaliwa katika mtaa wa Kano, kaskazini mwa Nigeria, polisi wamesema.

Naibu kamanda wa polisi Tasiu Ishaq alisema vijana hao waliovalia kama wanawake, walitiwa mbaroni siku ya Jumapili.

"Ni aibu kwamba wanaume na raia wema wanaweza kuwa na tabia kama hii na kujifanya kuwa wanawake," alisema.

Kamanda Ishaq alisema wanaume hao walikuwa "wamehubiriwa" juu ya athari za kiroho za matendo yao na wataachiliwa kwa wazazi wao.

 Mmoja wa watu walioshtakiwa aliiambia BBC kuwa rafiki yake alikuwa amemwalika kwenye sherehe hiyo na kwamba mtu ambaye ndiye mwenye sherehe alitoroka wakati polisi wa Kiisilamu walipofika.
 "Wametuhubiria na tumeomba tangu watukamate. Ninajuta kilichotokea na nitaacha tabia hii kwa neema ya Mungu, "alisema.

Kano ni moja wapo ya majimbo kaskazini mwa Nigeria ambayo inasisitiza Sharia, sheria ya dini ya Kiisilamu, ambayo imekuwa hapo tangu 2001.

Polisi wa Kiislamu wana nguvu ya kuwakamata watu wanaoamini kuwa wana vitendo ambavyo ni kinyume na sheria za Kiislamu.