SAKAJA

Kundi moja la wanasiasa wanaounga mkono mchakato wa BBI limekaribisha hatua ya wabunge wa Tanga Tanga kubadili msimamo wao kuhusu mikutano ya BBI.

Wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed na mbunge wa Kieni Kanini Kega walisema kwamba mikutano yao yote ni huru kwa wakenya wote.

Junet hata hivyo alihoji uamuzi wa wabunge wanaomuunga mkono naibu rais William Ruto kubadili msimamo wao wa awali na kutangaza kuungana nao katika mkutano wa Mombasa siku ya Jumamosi.

"Huwezi sema jambo fulani leo na kesho unabadili msimamo. Hii inachanganya wakenya," Junet alisema.

"Tunakaribisha wale wenzetu ambao roho mtakatifu ameingia kwa roho zao, wanakaribishwa kwa roho safi lakini mkuje na adabu. Unafiki wa kupanga mikutano mkabala na mikutano ya BBI na huku mnajifanya kuhudhuria mikutano ya BBI ndio tumechoka nao."

Sakaja alisema BBI ni ya Jubilee na ODM na wabunge wa tanga tanga wasije na masharti yao.

"Tunafaa kuwashukuru kwa kuona mwangaza na kuchagua kuungana na wakenya kutafuta kuwepo kwa amani nchini," Sakaja alisema.

Mbunge wa Kieni Kanini Kega alisema mkutano huo hautakuwa wa kisiasa bali fursa ya wakaazi wa Mombasa kutoa maoni yao kuhusu ripoti ya BBI. Alisema mikutano sawia na hiyo imepangiwa kufanyika katika maeneo mbali mbali ya nchi ili wakenya watoe maoni yao.

“Hii mambo si ya siasa. Sana sana ni kusikiza wananchi vile ambavyo wanasema. Kama hao watu kutoka mrengo mwingine wamesema watakuja Mombasa, kujeni msikize lakini usikuje na masharti,” Kanini alisema.

Junet alisema kwamba kundi linalomuunga mkono Ruto linadaiwa kupanga mikutano mbadala kote nchini.

“Ruto na wandani wake wamepanga njama kutwaa mikutano ya BBI na kuchukuwa usukani wa mchakato huo,” Junet alisema.

View Comments