RUTO ECHESA (1)

Naibu  wa Rais William Ruto ameendelea kujipata pabaya kuhusiana na sakata ya ulaghai wa ununuzi wa vifaa vya kijeshi kutoka kwa kampuni moja  kwa jina Echo Advanced Technologies baada ya kukamatwa kwa aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa . Ruto amekiri kwamba Echesa  aliwaleta katika afisi yake raia wawili wa kigeni kwa mkutano lakini hakufahamu lolote wala kukutana nao .

Maswali yanazidi kuibuliwa jinsi Echesa alivyoweza kuwaingiza raia hao wa kigeni katika afisi ya Ruto licha ya ulinzi mkali katika Jumba la Harambee Annex  na utaratibu mrefu wa mtu kujitambulisha na kueleza dhamira yake kuingia humo . Tayari Picha za CCTV zimethibitisha kwamba ni kweli Echesa aliingia katika jumba hilo pamoja na raia hao wa kigeni wa kampuni iliyofaa kuiuzuia Kenya zana za kivita . Sakata hiyo ya shilingi bilioni 40 inatishia kumpaka  tope naibu wa rais William Ruto ingawa hadi kufikia sasa hakuna ithibati inayomhusisha na njama yenyewe ila mkutano kufanyika katika afisi yake .

Siku ya jumapili ,Ruto kwa mara ya kwanza alikubali kwamba mkutano wa Echesa na wageni wake ulidumu kwa dakika 23 . Ruto ameonekana kuzishtumu pia afisi nyingine za serikali akishiria kwamba huenda  waliopanga njama hiyo pia walizuru  wizara ya Ulinzi . Echesa alikamatwa muda mfupi baada ya kuondoka afisi ya Ruto  na alisalia seli wikendi nzima .waziri huyo wa zamani anatarajiwakuachiliwa huru kwa dhamana ya shilingi milioni moja pesa taslimu  huku uchunguzi kuhusu  sakata hiyo ukiendelea. Baadhi ya viongozi wa kisiasa wameanza kumtilia shiniklizo Ruto  ang’atuke afisini kwa ajili ya sakata hiyo .  Gavana wa Kitui Charity Ngilu kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari amesema  Ruto amesaliti uaminifu wa wakenya milioni 47 kwa kujihusisha na sakata hiyo ya uuzaji feki ya silaha za kijeshi . Ngilu amesema vitendo vya Ruto vimeitia aibu afisi ya Rais.

 

View Comments