Kenya imesajili visa vinane zaidi vya maambukizi ya virusi vya korona na kufikisha jumla ya visa 15 ambavyo vimethibitishwa nchini Kenya.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema kati ya wanane hao kuna wakenya 5 na raia 3 wa kigeni na wote waliingia nchini kutoka nje. Amesema tayari wametengwa na hali yao ni thabiti isipokuwa mtu mmoja ambaye ni raia wa Ufaransa aliyekuwa ametengwa katika eneo la Msambweni.

Maafisa wa afya wanaendeelea na juhudi za kusaka takriban watu 300 waliokaribiana na wanane hao.

Kutokana na hali hii serikali imepiga marufuku safari zote za kimataifa za ndege za ifikiapo siku ya Jumatano. Ni ndege za mizigo pekee zitakazo ruhusiwa nchini.

Waziri anasema ni raia wa Kenya pekee na wale walio na vibali vya kuishi nchini Kenya watakaoruhusiwa kuja nchini hadi siku ya Jumatano. Mkenya yeyote ambaye hatakuwa amerejea nchini kufikia siku hiyo italazimika kusalia aliko. Kulingana na agizo la serikali mtu yeyote atakayewasili nchini atalazimika kujitenga kwa siku 14 kwa gharama yake.

Serikali vile vile imesema kwamba yeyote atakaye kaidi agizo la kujittenga atalazimishwa kufanya hivyo na kuplekwa mahakamani baada ya muda huo. Wakati huo huo serikali imetangaza kufungwa mara moja kwa makanisa na misikiti yote nchini na kwamba yeyote atakayekaidi agizo hili atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Serikali pia imeagiza kufungwa kwa baa zote kuanzia leo usiku. Hoteli zitaendelea kuhudumu lakini zimeagizwa kuwapakia wateja vyakula ili wakuliye nyumbani.

Kagwe vile vile amepiga marufuku mikusanyiko ya watu mahali popote pale iwe barabarani au sikoni.

Katibu wa kudumu wa usalama wa ndani Karanja Kibichu ameagiza maafisa wa utawala kuhakikisha kuwa masharti yote yaliotolewa na serikali yanatekelezwa bila kusita. Amesema Machifu na manaibu wao wanafaa kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kuabudu hayafunguliwi.

Katika masharti mapya mazishishi pia yatahudhuriwa tu na watu wa famila ya marehemu pekee na hawatazidi watu 15. Waziri Kagwe amewatahadharisha vijana wanaorejea nchini kutoka ng’ambo dhidi ya kukaribia wazazi wao wazee kabla ya siku 14 kuisha akisema kwamba virusi vya Corona vinaathiri sana watu wenye umri wa juu.

View Comments