‘Rogue Station’: Kayole Police, Kitovu cha maovu, wizi na mauaji ya kiholela
Ahadi inayotolewa na huduma ya polisi nchini Kenya ni ‘utumishi kwa wote ‘ na unatarajia kwamba kuna utu ,kujitolea, uaminifu na uadilifu katika utendakazi miongoni mwa polisi wa humu nchini .
Licha ya juhudi za kujaribu kuipa sura mpya huduma ya polisi na kuifanya iweze kuaminiwa na umma, huduma ya polisi nchini imezidi kujipata pabaya machoni mwa umma kwa kufuatia mienendo ya baadhi ya maafisa wake wasiotii sheria au kujali haki za kimsingi za binadamu. Kando na visa vya hivi karibuni tangu kutangazwa kwa marufuku ya kutotoka nje na kusababisha baadhi ya polisi kuwapa kipigo raia na hata kumuua mtoto wa miaka 13 katika mtaa kiamaiko, utovu wa nidhamu kwa upande wa polisi ni tatizo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu sana.
Iwapo kuna kituo cha polisi humu nchini ambacho kimechangia pakubwa kuwaharibia polisi sifa na utendakazi wao , basi kituo cha polisi cha Kayole, jijini Nairobi hakiwezi kusahaulika. Kwa sasa kituo hicho na maafisa wanaohudumu hapo wametajwa pakubwa kuhusiana na mauaji ya mshukiwa wa ujambazi aliyehusishwa na wizi wa shilingi milioni 72 katika mashine moja ya ATM Nairobi West, Wycliffe Vincent Owuor ambaye kifo chake wiki jana kimezua maswali kuliko majibu kwani ripoti za hali iliyosababisha kifo chake zinakinzana. Polisi wanasema aliuawa katika ufyatilianaji wa risasi na maafisa wa usalama lakini wakili wake Cliff Ombetta amedai kwamba mteja wake aliauawa kinyama.
Kabla ya kuibuka ripoti za uhusiano wa karibu kati ya Owuor na baadhi ya maafisa katika kituo hicho, kumekuwa na msururu wa maafisa wa polisi wa kituo hicho waliojipata katika mkondo mbaya wa sheria baada ya kuhusishwa na wizi wa kimabavu na mauaji ya kiholela na kituo hicho kinachunguzwa kwa visa kama hivyo.
Mmoja wa waathiriwa Daniel Wang’ombe alifariki Disemba tarehe 19 katika kituo hicho katika hali ya kutatanisha .Mwingine Magdaline Ombango alikamatwa na kuzuiliwa kituoni humo lakini akaaga dunia akiwa seli baada ya kudaiwa kuanguka . Mwaka uliopita maafisa wawili wa polisi kutoka kituo hicho walikamatwa kwa kuwa sehemu ya genge la majambazi waliomwibia mfanyibiashara mmoja wa eastleigh shilingi milioni 6 . Mmoja wa maafisa hao Simon Mwaniki baadaye alishtakiwa katika mahakama ya makadara kwa wizi huo .
Mwaniki pia alishtakiwa kwa wizi wa kimabavu baada ya kuhusishwa katika genge lililoiba shilingi milioni 2.7 kutoka kwa mwekezaji mmoja Wuwei Dun ambaye alikuwa kielekea Nakuru na wafanyikazi wake wawili na gari lao kusimamishwa na watu waliokuwa wamejihami akiwemo afisa huyo wa polisi. Kando na visa hivyo, Mamlaka ya Ipoa na kitengo cha kushughulikia lalama ndani ya Huduma ya polisi kinawachunguza polisi kadhaa kituoni humo kwa maovu mbalimbali .