Boy

Jeff Wechuli  amekuwa na maisha magumu  kwa miaka 17 tangu alipozaliwa kwa sababu pindi alipotimu umri wa miaka 12 aligundua kwamba wazazi wake aliokuwa akiishi nao sio wazazi wake wa kumzaa.

Inadaiwa wazazi hao wake wa kumlea ambao walikuwa wote wahadhiri wa chuo kikuu humu nchini hawakuweza kupata mtoto na wakaamua ‘kumnunua’ alipokuwa mdogo  katika hali ya kutatanisha ambayo imezua mgawanyiko mkubwa katika nafsi yake. Miaka 17 baadaye, ukweli kuhusu kilichomfanyikia umebainika na sasa kuna kesi inayoendelea  mahakamani kuhusu suala lake. Jeff aliibiwa kutoka hospitali moja ya kimishenari huko Tororo katika nchi jirani ya Uganda ambako mamake alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha nguo .

Babake alikuwa  meneja katika kiwanda hicho na  alipozaliwa, madaktari walisema aliaga dunia. Mamake alirejea Kenya baadaye katika eneo la  Naitiri, Bungoma  na kuendelea na maisha yake huku moyoni mwake akifahamu kwamba mtoto wake aliaga dunia. Kilomita kadhaa kutoka Naitiri, sehemu ya Chwele, kuna mtu na mke wake ambao walikuwa wahadhiri Nairobi na wasomi tajika katika jamii. Walikuwa ndio wameuziwa mtoto wa miezi miwili kutoka Uganda. Kitu ambacho hawakufahamu ni kwamba, mama mtoto halisi alikuwa Naitiri na alikuwa mkenya!

Yote yalifuchuka siku moja Jeff alipokuwa darasa la saba, baada ya mtihani wa muhula wa tatu kwenda darasa la nane, shangazi yake wa familia iliyomchukua  akiwa mdogo alimuambia kwamba hakuwa mtoto wa boma hilo na kwamba damu yake ni ‘geni’ kwani alikuwa ‘mganda’. Jeff alishangaa kwa sababu  shangazi yake hakuwa akifanya utani. Alipomuuliza mamake mlezi kuhusu hilo, aligundua kwamba mama yule alishtuka sana na hata akashindwa kuzungumza. Jeff papo hapo alifahamu kwamba kilichokuwa kikisemwa ni ukweli. Babake alipoambiwa kuhusu kilichofanyika alikuwa na hasira kupindukia na Jeff alishangaa iwapo  aliyosema shangazi yake yalikuwa uongo , mbona wazazi wake walikuwa na uchungu mkubwa hivyo kutaka kuficha jambo ambalo hakulijua. Jeff alimuambia mwalimu wake kuhusu kilichofanyika na mwalimu akamuunganisha na wakili wa shirika moja la kulinda maslahi ya watoto. Jeff hakuwa akiteswa na wazazi wake walezi lakini aligundua kwamba jamaa zake wengine  walikuwa wakimuona kwa njia tofauti. Hakuna aliyekuwa akimpa uzingatifu wowote na hata wakati wa mikutano ya familia , watoto wa kaka za  babake au mamake hakutangamana naye kama  mtoto wa familia ile. Hisia hiyo ya shauku ilisalia katika fikra yake hadi ukweli ulipolipuka

Shirika lililochukua kesi yake lilianza kufanya uchunguzi wa kisiri kuhusu wazazi halisi wa Jeff na baada ya miaka mitano baadaye, Jeff alikuwa ashajua anakoishi mamake na jinsi alivyoibwa kutoka Tororo na kuuzwa kwa wazazi wake wa sasa. Alichanganyikiwa asijue atafanya nini kwa sababu mamake mzazi sasa alikuwa mgeni kwake ilhali mamake mlezi hakuwa mamake halisi .

Akikaribia kutimu umri wa miaka 18 ili kuzingatiwa kama mtu mzima, Jeff aliweka chini ya utunzi wa shirika moja la makao ya watoto akingoja kufika umri wa kuamua iwapo atataka kurejeshwa kwa mamake  aliyemzaa au kusalia na wazazi wake waliomnunua .

View Comments