Siku moja katika siasa ni muda mrefu ambao unaweza kuibuka na mengi kama ulivyofahamu mrengo unaomuunga mkono naibu wa rais William Ruto  siku ya Jumatatu .

Baada ya washirika wake katika uongozi wa senate kutimuliwa, sasa ni dhahiri kwamba Ruto amekuwa akilengwa kuvunjwa miguu kwa muda sasa na yaoanekana mrengo wa rais Uhuru Kenyatta ulikuwa ukingoja wakati mwafaka wa kuanza kufanya mageuzi ya kumlemaza kisiasa. Awali wengi hawajakuwa wakiamini kwamba ushirikiano wa Kenyatta na Ruto umefika mwisho huku wafuasi wengi wa Jubilee wakijiliwaza kwamba hatua hiyo ilikuwa sehemu ya mkakati wa Kenyatta kuhakikisha kwamba baadaye anamuunga mkono naibu wake kuchukua usukani atakapoondoka mamlakani mwaka wa 2022. Huenda hilo ni kweli lakini jinsi migawanyiko inavyozuka na vilio vya kusalitiwa vikikithiri, huenda meli hiyo imeshang’oa nanga. Swali sasa ni je, naibu wa rais Ruto  ana chaguo gani bora wakati huu ili kuhakikisha kwamba anamrithi Kenyatta?

Wadadisi wamehoji uwezo wake kuweza kupiku  mfumo wa ndani ya serikali wenye ushawishi mkubwa ambao umeapa kuhakikisha kwamba hakaribii Ikulu . Mkondo wa kuwatumia wapiga kura kufika state house pia umeanza kukosa matumaini kwa sababu wengi sasa wameanza kuamini kwamba  sio uamuzi wa wapiga kura ambao uheshimiwa kuamua kiongozi wa  nchi  bali kundi la watu wenye ushawishi mkubwa kuweza kuendesha mfumo wa serikali.  Katka historia, Daniel  Moi pekee ndiye alaiyefaulu kuchukua usukani wa nchi baada ya kuhudumu kama makamu wa rais na ukisoma masimulizi ya masaibu aliyopitia kabla ya kufika hapo basi utafahamu kwamba DP Ruto aliteleeza kuanzia mwanzo. Kosa ambalo DP Ruto alifanya  wanasema wadadisi ni kuonyesha kichwa chake mapema kwamba alikuwa na nia ya kuchukua usukani. Kampeni za mapema za Ruto na hata hatua yake ya kuanza kuunda mitandao ya wafuasi hata katika ngome za mkuu wake zilimfanya kujenga uhasama thabiti wa chini kwa chini ambao sasa utakuwa mgumu kuuvunja wakati huu .

Ruto pia alijenga kikosi kikubwa cha maadui ambao sasa wakati huu wanamchekelea kwa masaibu yake kwani katika siasa hufai kuvunja kabisa daraja la maridhiano lakini kwake huenda amevunja madaraja mengi sana ili kufanya kuwa vigumu kuweza kuwavutia upande wake watu ambao wangemsaidia kukabiliana na zimwi la sasa la kumzuia kuingia Ikulu .

Wachanganuzi wanasema bado ni mapema sana kumpuuza Ruto kwani anaweza kunufaika na hali ya kisiasa inayobadilika kila kuchao. Endapo kutakuwa na muungano wa kupinga  azma yake ya kuwania urais, Ruto anaweza kunufaika na tofauti ambazo huenda zikaibuka katika muungano kama huo ili kusambaratisha wapinzani wake na kuweza kupenyeza ili kushinda vita vya kuingia Ikulu. Wengi wanamshauri Ruto kuwa mtulivu na kuanza kujenga upya mtandao wa wafuasi wake kutegemea viongozi ambao wana uzoefu  kinyume na mtindo wake wa sasa wa kuwatumia viongozi chipukizi wengi wasiokuwa na ushawishi bali payuka payuka za hapa na pale ambazo zinamzidishia uzito wa kuweza kuwashawishi watu wengi katika jitihada zake za kuingia  ikulu.

View Comments