mans

 Sio lazima umuambie  mtu kwamba unampenda ili ajue kwamba kweli unamuenzi. Kuna vitu au vitendo ambavyo vitatuma ujumbe huo kwa njia ya wazi sana  tena ya kuvutia kumuonyesha kwamba unampenda na unamjali. Katika ulimwengu wa sasa  ambao una mkimbizo wa  kila aina katika maisha, wakati mwingine inakuwa vigumu kupata fursa ya kuweza kutamka neno hilo  ‘nakupenda’. Hizi hapa baadhi ya njia za kuweza kumfanya mwenzako ajue kwamba unampenda

 1.Mpe muda wako

Tumia fursa unayopata kuwa naye. Na sio tu kuketi sebuleni na kuwasha runinga ili kuona filamu pamoja, hapana.Zima TV, weka simu yako kando na  muangalie mwenzako tu mkisemezana. Tembeeni pamoja hata kwenda kupata chakula hivi.  Jipeni shughuli nyinyi wawili tu ili muwe na fursa ya kucheka na hata kuzua kumbukumbu ya mambo ya zamani. Hili hufanya miujiuza sana kwa sababu muda unaotumia kutangamana na  mtu ndio huzua fikra za muda wenu mzuri nyakati za baadaye.

2. Jiwekee vikumbusho au  Reminders.

Siku hizi itakuwa vigumu kutegemea fikra zako kukumbuka tarehe muhimu za kuweza kumshtukizia mwenzako kwa jambo ama kitendo cha kumfurahisha. Kwa sababu ya hilo, ifanye teknolojia kuwa rafiki wako wa karibu, weka vikumbusho katika kalenda na katika simu yako ya rununu ili ujue siku ipi kumnunulia bunda safi la maua, siku ya kumshtua kwa keki nzuri ya ndizi akiwa afisini au nyumbani, siku bora kwake kumpeleka mkahawani kwa chakula au hata siku maalum ya kumpeleka kidimbwini aogelee .

3.Msikilize bila kumpa ushauri au kutoa maoni yako 

Hakuna  kizuri kwa mwanamke kama kumzikiliza na hata kuzingatia yote anayosema bila kuingilia au kutoa ushauri. Mpe muda wako  anaposema yote  atakayo. Sikiliza na iwapo hata utaingiza maigizo kwa kujifanya  umefungua sikio ili  uyapate maneno yake yote  basi fanya hivyo. Kuwa na mtu  anayeweza kukusikiliza ni hatua ambayo huzua hisia ya utegemezi. Anafahamu fika kwamba licha ya matatizo yote nayopitia, kuna mtu atakayenisikiliza na kunielewa.

4. Jifunze kuomba msamaha

Watu wengi hawajui jinsi ya kuomba msamaha wakati wanapokosea. Lakini ili kuonyesha kwamba unajali na unampenda, hakikisha kwamba njia yako ya kuomba msamaha ni ile inayofaa. Kujua kuomba msamaha kutuepusha makovu na mvutano wa kila mara. Vigezo muhimu vya kuomba msamaha ni kuhakikisha kwamba unajutia kosa lako, unaahidi kurekebika, unaapa kuwajibikia kosa lako  na kisha kuomba  msamaha

5. Salimu amri

Amekuwa akitaka ufanye jambo fulani jinsi anavyotaka, usikate. Mpe ushindi wake naye ahisi kupendwa. Hataki utafune  jinsi hii basi rekebisha na ufanye anavyotaka. Hapendi uvalie shati lako unalopenda kwa sababu limechubuka rangi au limeanza kuchanika, mkubalie kwa kulitosa shati hilo. Hatua ya kufanya hivyo ni kumfanya ajue kwamba  unamthamini sana kuliko vyote unavyopenda.

6 .Mpe usaidizi pale nyumbani

Kumsaidia mwenzako ni  kutuma ujumbe kwamba ‘sote pamoja tupo katika hili’. Mwanamme kumsaidia mwenzako pale nyumbani kwa kazi za hapa na pale  sio udhaifu bali ni ujasiri wa kuweza taarifa nzito kwamba unamjali na mazito yake ni yako pia. Imekuwa dhana ya kupotosha kwamb  kazi zote za nyumbani ni za mwanamke, hili lina athari ya kuzua hisia za mwenzako kujiona kama kijakazi wako. Onyesha kujali kwa kuchangia kumpunguzia mzigo pale hata kwa kutoa jaa la taka au kujifunga kibwebwe na kuingia jikoni. Hata kama ni kuchemsha  chakula alichopika tayari.

7. Ijali familia/jamaa zake

Kuonyesha kujali kwa familia yake ni hatua inayotuma ujumbe kwamba wewe sio mgeni wa kupita. Taka kuwajulia hali jamaa zake au hata watu ambao ni muhimu katika maisha yake. Uliza maswali kuhusu hali zao. Mamake ni muhimu sana katika maisha yake kwa hivyo hakikisha kwamba una ufahamu  wa kinachofanyika upande wa pili. Hatua hiyo humpa mwanamke  usalama wa aina fulani kujua kwamba kuna mtu ambaye anazingatia maslahi ya watu wake na sio tu yeye pekee.

8.Mruhusu akushawishi

Mara sio moja, jaribu kuangalia mambo kwa mtazamo wake. Kubali pendekezo lake hata iwapo una pendekezo bora. Ni vizuri kuwa sawa wakati wote lakini kuna ubora wa kudumu iwapo mwenzio atakuwa na furaha kwa sababu umekubali kuchukua hatua inayompa tabasamu. Iwapo kuna jambo ambalo umekua ukijiamulia au ukifanya kwa namna yako, jaribu kupata maoni yake akupe njia mbadala unayoweza kufanya jambo hilo, hilo litampa raha sana kwani atajihisi amechangia pakubwa katika  ufanisi wenu.

  1. Taka kujua zaidi

Usionyeshe kuridhika na yote unayojua kumhusu mwenzako. Taka kujua mengi zaidi katika kumbukumbu na fikra zake. Kuuliza amswali kuhusu maisha yake ya utotoni ni jambo ambalo litamfanya kujihisi mwenye thamani kwako. Endapo utajipata huna unalotaka kujua kumhusu mwenzio kwa sababu mmekuwa pamoja kwa muda mrefu, huenda uhusiano wenu umepiga breki na hamwezi kujua mmefika wapi katika kujiboresha kwa kila njia. Kutotaka kujua zaidi kumhusu mwenzio pia hutoa dhana kwamba umechoka naye.

 10 .Muulize kinachofanya ahisi kupendwa

Wakati mwingine, njia bora ya kufanya kitu ni ile iliyo wazi. Kwa hivyo, badala ya kubahatisha na kucheza kamari, muulize mwenzako anapenda nini, anataka kufaniwa kipi? Unaweza kujitahidi  kumnunulia maua kila wakati kumbe hapendi yanavyonukia au hapendi maua licha ya kwamba yanavutia.

 

View Comments