Wakili mmoja eneo bunge la Funyula kaunti ya Busia amekashifiwa na mwanamke mmoja kwa kutoweka na KSh 1.6 milioni ambazo alikuwa amelipwa kama fidia.

Jackline Nakholi mwenye umri wa miaka 27 alihusika katika ajali ya barabara mwaka wa 2014 eneo la Ugunja katika barabara kuu ya Busia-Kisumu.

Nakholi na mwanawe walilazwa katika hospitali ya Kisumu ambapo mwanawe alikatwa mguu wa kulia.

Baada ya kupona, Jackline alianza kutafuta haki kupitia kwa wakili David Neriko Omwengo ambaye alimwakilisha katika kesi hiyo iliyochukua miaka mitatu kutatuliwa.

Mwanamke huyo alishinda kesi hiyo ambapo familia ilifidiwa KSh 1.6 milioni, mtoto KSh 1.1 milioni na mwenyewe KSh 550,000.

" Mtoto wangu alikuwa awekewe mguu mwingine, hatuna fedha za kugharamia matibabu haya yote, ningependa Mkuu wa Mashtaka na mkurugenzi wa Upelelezi DCI waingilie kati watusaidie tupate haki," Nakholi alisema.

Juhudi za kumtafuta wakili huyo hazijafaulu kufikia sasa na imempelekea mwanamke huyo kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

Wakili huyo anasemekana kumualika mama huyo afisini mwake na kumuahidi kumlipa KSh 1.2 ikizingatiwa pia alitaka kulipwa kwa kusukuma kesi hiyo hadi akashinda.

View Comments