05 June 2020 1 Min Read
Waziri mkuu wa Uganda ajiweka karantini baada ya kutangamana na watu waliopatikana na corona
by Grace Muia Habari
Waziri Mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda amejiweka karantini baada ya watu aliotangamana nao kupatikana na virusi vya COVID-19.
Rugunda alisema hakupatikana na virusi hivyo baada ya kupimwa ila ameonelea ni vyema kufuata masharti yaliowekwa ya kudhibiti maambuki ya virusi hivyo.
" Marafiki zanguni, nimeamua kujitenga kwa siku 14 baada ya watu niliotangamana nao kukutwa na virusi vya COVID-19, mimi mwenyewe sijapatikana na virusi hivyo lakini nafuata masharti yaliowekwa na wizara ya afya ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu," Alisema Rugunda.
Wizara ya afya nchini humo Alhamisi, Juni 4 ilitangaza kuwa sampuli 2,267 zilifanyiwa vipimo na visa vyote ni vya raia wa Uganda.
Kufikia sasa nchi hiyo imethibitisha visa 35 vipya vya maambukizi ya virusi vya COVID-19 chini ya saa 24 zilizopita na kufanya idadi ya walioambukizwa kufikia 557.
Aidha, madereva 31 wa malori, 18 wakiwa Wakenya, 7 Watanzania, 4 Wakongo na 2 Waburundi waliopatwa na virusi hivyo walirejeshwa makwao.