Je, Uhuru na Raila wanapanga kumuunga mkono Mukhisa Kituyi kuwania urais 2022?
Mukhisa Kituyi huenda akawa mgombeaji wa siri wa urais ambaye rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga wanapanga kumuunga mkono katika uchaguzi wa mwaka wa 2022, kwa mujibu wa washirika wa karibu wa viongozi hao wawili .
Wameliambia gazeti la The Star kwamba waziri huyo wa zamani wa biashara anazingatiwa kwa nafasi hiyo endapo Odinga hatogombea urais kwa mara nyingine.
Kuna uwezekano wa odinga kujitosa tena ulingoni kwa mara ya nne lakini hajathibitisha hilo. Inafahamika kwamba rais Uhuru Kenyatta anamzingatia Kituyi kama mtu anayeweza kumrithi kwa sababu ya uzoefu wake kisiasa na hadhi yake ya kimataifa.
Uhuru pia anaripotiwa kumzingatia kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi kama anayeweza kumrithi. Kituyi kwa sasa ni katibu mkuu wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu biashara na maendeleo (Unctad) na kipindi chake cha kuhudumu kitamalizika Julai mwaka wa 2021.
Malumbano katika chama cha Ford Kenya yamehusishwa na kurejea kwake ili kuchukua usukani kabla ya uchaguzi.