Jamaa mwenye umri wa miaka 35 kutoka Kijiji cha Sigaon kata ya Neisuit, Kaunti ya Nakuru aliaga dunia Jumatatu Juni 15 usiku baada ya kusakamwa na kipande cha nyama.

Marehemu, aliyetambuliwa tu kama Rasta, alirejea nyumbani saa kumi na moja jioni Jumatatu akiwa amelewa chakari jinsi majirani walisema

"Alikuwa mlevi na alilalamikia njaa," jirani mmoja alisema.

Mwenyekiti wa Vijana wa Neisuit, Kitur Sigei, alisema Rasta alikuwa amebeba nyama iliyofungwa kwenye karatasi ya gazeti, wakati alipofika nyumbani.

"Akiwa katika hali ya kuchemsha nyama hiyo, alianza kuila kabla haijapikwa vizuri," alisema Sigei.

"Kwa bahati mbaya alisakamwa. Majirani walimsikia Rasta akiitisha msaada. Walipokimbia nyumbani kwake walimkuta akigaagaa kwa maumivu makali. Mmoja wa majirani alijaribu kumsaidia ili akitapike kipande hicho lakini juhudi zake hazikufaulu," Sigei alikariri.

Majirani hao waliamua kumkimbiza katika kituo cha afya kilichoko karibu lakini alipowasili tayari alikuwa amekata kamba.

Rasta alijishughulisha na vibarua vya hapa na pale ili kujipatia kipato, hakuwa na mke au watoto, na majirani sasa wanaiuliza serikali ya kaunti iwaruhusu wamzike katika eneo hilo.