-FgregsW.jfif

Uhasama wa muda kati ya wanamuziki Bahati na Willy Paul kwa sasa ni ya kale na wanaganga yajayo baada ya wawili hao kuzika tofauti zao.

Wawili hao wamekuwa wakikwaruzana hadharani tangia mwanzo wa taaluma zao za muziki.

Bahati, huku akimtaja Pozee kama kaka yake alifichua kwamba kwa sasa Willy Paul ni rafiki yake wa kufa kuzikana na huwa wanawasiliana kila wiki.

“Huyu ndugu yangu Willy nampenda sana, hata juzi nilikuwa na yeye. Ni ufala tuu anakuwanga nayo, huwa tunazungumza kila wiki na kutembeleana studioni. Hakuna uhasama hiyo ilikuwa utoto ya kitambo,” Bahati aliambia Nairobi News katika mahojiano.

Wasanii hao wawili wamekuwa wakishindana kila mara na kugombana wakati wa hafla za tuzo za muziki.

Willy Paul ambaye awali alikuwa mwimbaji wa nyimbo za injili, aligura mtindo huo na kuanza kuimba nyimbo za kidunia.

Na Bahati sasa anadai kutumia uhusiano wao mpya kumrejesha Willy Paul katika nyimbo za injili na kusisitiza bado ni msanii wa injili licha ya wimbo wake wa Wanani ambao umezua hisia kinzani.

“Wimbo wa Wanani sio wa Injili lakini haimanishi kwamba ninajiunga na nyimbo za kidunia," alibainisha Bahati.