Janga la corona limevuruga maisha ya wengi kuliko mtu yeyote angevyoweza kujua lakini sasa jinsi ugonjwa huo unavyozidi kueleweka na athari zake inabainika wazi kwamba itakuwa kazi ngumu na muda mrefu  kuweza kukabiliana na  madhara ya ugonjwa huo .

Watu wanavyozungumzia  kuhusu  jinsi  ugonjwa wa corona ulivyowafanya wengi kupoteza kazi zao ,hakuna wanaofikiri kuhusu baadhi  ya kazi  kama vile za nyumbani na  nyingine katika sektaya jua kali .  Tangu kuanza kwa janga hilo maelfu ya wafanyikazi wa nyumba waliachishwa kazi na waajiri wao kwa sababu ya kutohityajika kwa huduma zao . watoto ambao hutunzwa na wafanyikazi wa nyumbani wamekuwa nyumbani kwa miezi mitatu na wazazi wao ambao wengi wao pia hawajakuwa wakienda kazini na hivyo basi kutohitaji mtu wa kuwatunza wanao .

Emily  Jerop anasema pindi mwajiri wake alipoanza kufanyiakazi nyumbani ,alimuambia kwamba hana pesa za kumlipa mshahara na kumtaka atafute pa kwenda .Ilikuwa   vigumu kwake kutafuta pa kwenda ikizingatiwa kwamba muda mfupi baadaye serikali ilitangaza marufuku ya kusafiri kutoka na kuingia jijini . Hangeweza kurejea mashambani na kwa sasa anamfanyia kazi bure mwajiri wake malipo yake kwa sasa yakiwa chakula na mahali pa kulala . Masaibu hayo hayajamkumba Emily pekee yake kwani visa ni vingi vya wafanyikazi wa nyumba ambao sasa  wameachishwa kazi kwa ajili ya waajiri wao kukosa pesa za kuwalipa mishahara .

Derick Onsando anasema yeye na mkewe walilazimika kumuachisha kazi mfanyikazi wao wa nyumbani wakati mkewe alipofutwa kazi kwa ajili ya c0vid 19 . Alikuwa akifanya kazi katika hoteli moja jijini ambayo ilifungwa wakati visa vya corona vilipoongezeka nchini . Alilazimika kurejea nyumbani kuwatunza wanawe  na kufanya kuwa vigumu wao kuendelea kuwa na mfanyikazi wa nyumba .

Priscilla  Khamala naye alilazimika kumuachisha kazi mfanyikazi wake wa nyumba kwa sababu  alihamia nyumba ndogo ili aweze kumudu kulipa kodi .‘Kabla ya Corona nilikuwa katika nyumba ya vumba vitatu vya kulala,mfanyikazi wangu alikuwa akilala  na dadangu katika chumba kimoja ,sasa baada ya biashara yangu kuvurugika ,siwezi kulipia nyumba kubwa hivyo na nimelazimika kuhamia nyumba ya chumba kimoja cha kulala’  anasema.

View Comments