Wafanyakazi walio katika mstari wa mbele haswa wahudumu wa afya, maafisa wa polisi na walinzi wa magereza, wamehimizwa kuvalia mavazi ya kujikinga dhidi ya maambukizi wanapotekeleza majukumu yao ili kujikinga dhidi ya maradhi ya Covid 19.

Katibu msimamizi wa afya, Rashid Aman amesema wote hao wamepewa mafunzo ya kutosha kuhusiana na ugonjwa huu. Hii inajiri ikidaiwa kuwa maafisa watatu kutoka kituo cha polisi cha Kamukunji wamepatikana na virusi vya Corona.

Wizara ya vijana na masuala ya jinsia imewasilisha shilingi milioni 44.2, fedha za msaada wakati huu wa janga la Corona kwa vijana na wanawake wanoishi katika mitaa ya mabanda.

Fedha hizo ni za kutoka kwa mashirika ya Women Enterprise Fund na Uwezo ambazo zitatumika kufaidi biashara za wanawake na mradi wa Kazi mtaani unaowaajiri vijana kutoa huduma mbali mbali katika mitaa yao.

Maafisa wa upelelezi wamewakamata watu watano wanaoaminiwa kuhusika na msururu wa visa vya wizi wa mabavu na mauaji ya mfanyibiashara mashuhuri katika eneo la Bungoma waliyemuibia shilingi milioni mbili.

Vile vile walinasa vifaa vingine vya thamani ya shilingi elfu 62. Wote hao wametiwa kizuizini.

Tunastahili kukabiliana na vishawishi vinavyowapelekea vijana kujiingiza katika uhalifu kama wale wanaowaandalia soko la kuuza bidhaa za wizi. Mtaalamu wa masuala ya usalama George Musamalu anasema wazazi na jamii vile vile ni wa kulaumiwa kwa kutoingilia kati na kuwakosoa wanao wanapojihusisha na visa vya uhalifu .

View Comments