- jm
- tom mboya
- tom.mboya
- ROBERT.OUKO.STAR
- MUGE
- JACOB JUMA

Wahenga walisema kwamba, kwa muoga huenda kicheko na kwa shujaa huenda kilio, lakini katika maisha yake muoga hufa mara kadhaa kabla ya kifo chake halisi kutimia.

Katika historia ya Kenya ni mashujaa wengi sana tuliowapoteza sio kutokana na maradhi bali kutokana na mtutu wa bunduki. Jambo linalokera sana ni kwamba kufikia sasa zaidi ya miaka 50 tangu wengine wao wauawe bado hatujategua vitendawili vya Vifo vya mashujaa hawa wa kutetea haki za kibinadamu.

Familia zao zimesamia na maswali mengi bila kupata majibu. Wengi wakisalia na kumbukumbu tu za wapendwa wao huku wakitafakari mateso waliyopitia kabla ya kukata roho.

Swali ni je, ni nani atakayetegua vitendawili vya mauaji ya mashujaa hawa ambao maisha yao yalisitishwa kwa lazima kwa mkono wa binadamu?

Tutaangazia tu baadhi ya mashujaa ambao vifo vyao viliguza nyoyo za wananchi na kufikia sasa familia zao bado zinasaka haki.

JM Kariuki

Josiah Mwangi Kariuki maarufu JM Kariuki alikuwa mwanasiasa shupavu na alihudumu katika serikali ya mtangulizi wa taifa la Kenya hayati mzee Jomo Kenyatta. Machi tarehe 2, Mwaka 1975 ilikuwa siku ya mwisho ya JM kuonekana akiwa hai, wakati huo alikuwa anahudumu kama waziri msaidizi.

Baada ya siku nne bila kujulikana alikokuwa baadhi ya wabunge waliitaka serikali kueleza alikokuwa JM. Familia yake ilianza kuuliza maswali na hofu ikatanda kote nchini. Ili kutuliza hofu iliokuwa imekithiri nchini serikali ya hayati mzee Jomo Kenyatta kupitia makamu wake wa rais marehemu Daniel Arap Moi iliambia bunge kwamba waziri msaidi JM Kariuki alikuwa ameenda safari ya kikazi nchini Zambia. Madai hayo hata hivyo yalikanushwa vikali na familia yake iliyodai kwamba JM hakuwa amesafiri nje ya nchi.

Hali ya huzuni iligubika taifa baada ya mwili wa JM Kariuki kupatikana siku chache baadaye katika milima ya Ngong na wafugaji wa kimaasai waliokuwa wakichunga ng’ombe. Mwili wake ulikuwa umechomwa na kutupwa. Kamati maalum iliochunguza kifo chake ilimhusisha afisa mmoja wa cheo cha juu katika idara ya polisi, hata hivyo kufikia sasa hakuna hatua iliochukuliwa dhidi ya mhusika yeyote katika mauaji hayo ya kinyama. Familia yake bado inasubiri na kuomba kwamba siku moja mbingu itafunguka na siku ya kiama aliyehusika na mauaji ya kinyama ya mbunge, bwana na baba JM Kariuki atahukumiwa mbele ya Mungu.

Tom Mboya

Thomas Joseph Odhiambo Mboya alikuwa moja wapo wa viongozi chipukizi katika serikali ya hayati mzee Jomo Kenyatta. Tom Mboya kama alivyojulikana na wengi alikuwa na weledi wa kutoa hotuba za kuvutia na alisikizwa na wengi. Alizaliwa mwaka 1930 na kuauwa katika 1969. Alikuwa miongoni mwa wataalam waliongoza mashauriano ya kuipa Kenya uhuru katika kongamano la Lancaster House. Tom Mboya alisaidia sana kuanzishwa kwa vuguvugu la kutetea wafanyikazi nchini na kupelekea kubuniwa kwa muungano wa COTU.

Weledi wake katika kutoa hotuba uliunua sana umaarufu wake na kutikisa ulingo wa kisiasa nchini Kenya na kimataifa. Lakini sio wengi walifurahishwa na umaarufu na ushawishi wake. Tarehe 5 Julai 1969 wakati huo akihudumu kama waziri wa Mipango na Maendeleo ya kitaifa, alikuwa ameenda kununua dawa katikati mwa mji wa Nairobi katika barabara iliyojulikana kama Government Road (Kwa sasa Moi Avenue) alipigwa risasi na kufariki muda mchache baadaye.

Mauaji yake yalitikisa uongozi wa hayati mzee Jomo Kenyatta. Nahashon Isaac Njenga Njoroge alipatikana na hatia ya kumuua Mboya na kuhukumiwa kunyongwa. Kulingana na serikali Njenga Njoroge alinyongwa lakini kulingana na wandani wa marehemu Mboya alitoroshwa nchini.

Itakumbukwa kwamba baada ya kukamatwa Njoroge aliuliza “why don’t you go after the big man” (mbona msiendee mkubwa). Usemi wake mtuhumiwa uliacha wengi na maswali ambayo hadi sasa majibu hayajapatikana.

Robert Ouko

John Robert Ouko alihudumu katika serikali za rais muanzilishi wa taifa la Kenya hayati mzee Jomo Kenyatta na marehemu rais Daniel Moi. Alizaliwa mwaka 1931 na kufariki mwaka 1990. Wakati wa kifo chake alikuwa akihudumu kama waziri wa mashauri ya nchi za kigeni.

Ouko aliripotiwa kutoweka nyumbani kwake eneo la Kinoru, Kisumu mnamo Februari mwaka 1990. Alikuwa tu amerejea nchini kutoka ziara ya kikazi aliokuwa amendamana na rais Daniel Moi nchini Amerika. Alikuwa miongoni mwa ujumbe wa watu 83 wakijumuisha mawaziri na maafisa wengine wakuu wa serikali waliondamana na rais Moi kwa mkutano mjini Washington DC.

Alitoweka nyumbani kwake usiku wa kuamkia Februari 13 na mwili Wake kupatikana katika milima ya Got Alila. Mwili wake ulikuwa umechomwa kwa kile wachunguzi walisema ulichomwa na tindi kali au asidi. Baadhi ya wafanyikazi katika boma lake walikiri kusikia mlango wa nyumba yake ukigongwa na kisha wakaona gari jeupe likisongea eneo lake la kuegesha magari.

Chunguzi kadhaa zimefanyika kubaini chanzo cha kifo cha mwanasiasa huyo na ni akina nani waliohusika. Cha kushangaza ni kwamba mashahidi wengi katika uchunguzi wa mauaji yake walifariki katika njia za kutatanisha wakiwemo waliyoupata mwili wake katika eneo la Got Alila.

Washukiwa wengi akiwemo aliyekuwa waziri mwenye ushawishi katika iliyokuwa serikali ya hayati mzee Moi, marehemu Nicholas Biwott walitajwa kuhusika katika kifo chake. Marehemu Biwott hata hivyo alikana madai yote kuhusiana na kifo cha Ouko.

Kufikia sasa uchunguzi wa kifo cha Robert Ouko bado haujakamilika, familia yake kila kunapo kucha huomba dua kwamba waliohusika watashikwa na haki kutendeka.

Chris Msando

Christopher Msando alikuwa meneja mkuu wa teknolojia ya mawasliano katika tume huru ya uchaguzi na mipaka - IEBC. Jukumu lake kuu lilikuwa kusimamia mfumo wa dijitali wa kupeperusha matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka 2017 ili kuhakikisha kuwa hakuna udanganyifu katika uchaguzi huo.

Alitoweka Julai 28 2017, siku ya Ijumaa na hata baadhi ya wanasiasa wakafanya utani kuhusu kutoweka kwake. Kulingana na ripoti ya uchunguzi mara ya mwisho gari lake lilionekana kwenye barabara kuu ya Thika.

Mwili wake uliyokuwa na majeraha ishara ya kuteswa kabla ya kuuliwa ulipatikana siku ya Jumamosi katika msitu wa Muguga kaunti ya Kiambu na maafisa wa polisi waliopeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City mjini Nairobi bila kujua kwamba ulikwa wa Msando.

Baada ya saka saka kila mahali mwili wake uligunduliwa siku ya Jumatatu baada ya kutambuliwa na jamaa zake.

Kulingana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Msando alikuwa ameteswa sana kabla ya kuauwa. Ripoti za ujasusi zaonyesha kwamba Msando aliuawa kwa kunyongwa baada ya kupigwa na kuteswa. Alikuwa amepambana na vikali na wauaji wake kabla ya kumzidi nguvu. Kifo chake kilizua hali ya taharuki nchini huku zikiwa zimesalia siku chache kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya.

Kifo chake kiliyumbisha sana tume ya IEBC na kutilia shaka uazi wa uchaguzi huo mkuu. Uchaguzi huo hata hivyo ulifutiliwa mbali na mahakama ya upeo kwa madai ya kukosa uazi na kuwepo kwa dosari chungu nzima. Licha ya asasi za serikali kuahidi kutanzua kifo chake, kufikia sasa hakuna aliyetuhumiwa kuhusiana na kifo chake.

Maswali ambayo bado familia yake na wakenya wanajiuliza ni je, Nani aliua Msando, kwa sababu gani na ni lini haki itatendeka?

Bishop Alex Muge

Bishop Alexander Kipsang Muge alikuwa mkosaji mkuu wa utawala chama cha Kanu. Munge na askofu mwenzake wa Maseno Kusini John Okullu walikuwa wametoa taarifa wakimtaka hayati rais Daniel Moi Kujiuzulu. Msimamo wake uliwakwaza baadhi ya wandani wa rais Moi na hata kupelekea aliyekuwa waziri wa Leba ambaye sasa ni marehemu Peter Okondo Khabenga kumuonya dhidi ya kuzuru Busia Agost 12 1990.

“They will see fire and may not leave alive (Wataona moto na huenda wasiondoke wakiwa hai),” Kondo alisema.

Siku iliyofuta Muge alimjibu Okondo akisema kwamba

“Let him know that my innocent blood will haunt him forever and he will not be at peace for God does not approve murder (afahamu kwamba damu yangu isiokuwa na hatia itamuandama maisha yake yote na hataona amani kwani Mungu haungi mkono kuua).”

Siku mbili baadaye Bishop Muge aliamua kwenda Busia na akiwa njiani gari alimokuwa akisafiria pamoja na wenzake likagongana ana kwa ana na lori la akafariki papo hapo.

Uchunguzi ulidai kwamba alifariki katika ajali ya kawaida na dereva wa lori lilogongana na gari lake akahukumiwa miaka saba gerezani lakini akafariki akiwa gerezani kabla ya kumaliza kifungo chake baada ya kuhudumu miaka mitano.

Mwaka 2012, aliyekuwa Inspekta katika kikosi cha Special Branch James Kwatenge aliambia tume ya kitaifa ya ukweli haki na maridhiano kwamba ajali iliyomuua Bishop Muge ilipangwa na kikosi maalum cha usalama kwa jina ‘Operation Shika Msumari’

Baadhi ya viongozi ambao vifo vyao vinakisiwa kutokana na uhasama wa kisiasa na ambavyo bado uchunguzi haujaeleza kinagaubaga kuhusu kiini cha mauaji yao kutaja tu wachache ni;

Pio Gama Pinto, aliyeuawa mwaka 1965,

Mfanyibiashara Jacob Juma aliyeuawa mwaka 2016 na ambaye alikuwa mwepesi sana kuzungumzia ufisadi katika serikali bila uoga, aliuawa kwa pigwa risasi.

Aliyekuwa mbunge wa Juja George Thuo aliuawa kwa kepewa sumu mjini Thika mwaka 2013 kulingana na ripoti za ujasusi.

Aliyekuwa mbunge wa Kabete George Muchai ambaye pia alipigwa risasi mwaka 2015 akiwa na walinzi wake.

Je vitendawili kuhusu mauaji ya wakenya hawa vitateguliwa au familia zao na wakenya kwa jumla watasubiri hadi siku ya kiama kujua ni nani na ni kwanini mashujaa hawa walikufa mikononi mwa binadamu wenzao.

View Comments