- Uhuru.jeshi.1
- uhuru.jeshi.4

Idadi ya wanawake wanaojiunga na jeshi la Kenya imeongeza marudufu katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Alhamisi alisema anaridhishwa na idadi inayoongezeka ya wanawake wanaojiunga na Jeshi la Taifa akisema kwamba jitihada zake akiwa Kiongozi wa Taifa ni kuhakikisha nafasi sawa kwa Wakenya wote.

"Ni muhimu kwa wanawake hawa wachanga, wakishirikiana na wanaume kutafuta maana na malengo kazini mwao. Wakati vijana hawa walipojiunga na Jeshi la Taifa kutoka sehemu zote za nchi hii tukufu, walijiunga kuwa familia yenye mshikamano," kasema Rais.

Matamshi ya rais kuhusu usawa wa jinsia yalijiri siku mbili tu baada ya jaji mkuu David Maraga kumshauri rais Kenyatta kulivunja mbunge kwa kushindwa kupitisha sheria ya kutekeleza usawa wa jinsia.

Rais Kenyatta ambaye alikuwa mgeni wa heshima katika gwaride ya kufuzu kwa wanajeshi mjini Eldoret, aliwashauri wanajeshi wapya, kuzingatia utaalam na uzalendo kuliko mengine yote wanapotekeleza wajibu wao wa kulinda nchi.

"Tunawapa wajibu wa kulinda taifa hili dhidi ya wavamizi na maadui... Mafunzo ambayo mumepokea ni ya kuwapa uwezo wa maarifa muhimu kutatua tatizo hili....Nawahimiza muwe stadi na wazalendo wakati wowote ule," Rais aliwaambia wanjeshi hao wapya wa kike na kiume.

Kama sehemu ya sherehe hizo kabambe zilizohudhuriwa na wakuu wote wa Jeshi wakiongozwa na Mkuu wa Majeshi Jemedari Robert Kariuki Kibochi, Rais aliwatunuku zawadi makurutu waliotia fora katika mafunzo yao ya miezi hiyo minane.

Gabriel Kipanga pamoja na Lawrence Mutua kutoka Kikosi cha Jeshi la Nchi Kavu ni miongoni mwa waliotuzwa kwa kushikilia nambari ya kwanza na ya pili mtawalia ilihali Miriam Cherono wa Kikosi cha Jeshi la Wanamaji alijizolea tuzo la kuibuka bora miongoni mwa wanawake. Brian Njeru kutoka Kikosi cha Jeshi la Wanamaji alishinda tuzo la mlenga shabaha bora zaidi katika ustadi wa mbinu za kivita.

View Comments