Polisi katika eneo la Kilimani jijini Nairobi wanachunguza kisa ambacho baba, mama na kaka wa msichana wa miaka 15, wanashukiwa kumpiga hadi kufa Alhamisi usiku kwa kukimbia nyumbani.

Wanandoa hao na mtoto wao walikamatwa baada ya msichana huyo kufariki hospitalini.

Afisa wa kliniki katika hospitali ya Coptic aliwaambia wapelelezi kuwa mnamo Mei 20 mwendo wa saa 9 usiku, hospitali hiyo ilipokea mgonjwa wa miaka 15, ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya upili ya ya Wasichana ya Kiteta huko Mbooni, Kaunti ya Makueni.

Alikuwa ameandamana na baba yake kwa uchunguzi wa matibabu baada ya kudaiwa kukimbia nyumbani na kukosa kuripoti shuleni.

Walakini, saa za Ijumaa, msichana huyo alikimbizwa katika hospitali hiyo hiyo baada ya kudaiwa kuanguka nyumbani kufuatia kipigo kikali kutoka kwa baba yake, mama yake ambaye anafanya kazi katika uwanja wa maonyesho wa ASK na kaka mkubwa wa msichana ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha TUK.

Kulingana na polisi, aliaga dunia baada ya kufika hospitalini.

Afisa wa kliniki alisema mwili wake wote ulikuwa na michubuko, ishara kwamba alikuwa ameshambuliwa vibaya.

Maafisa wa upelelezi kutoka DCI Kilimani waliotembelea eneo la tukio walipata bomba moja ya PPR iliyotumika kumpiga msichana huyo.

Wakati uchunguzi zaidi ukiendelea, washukiwa hao watatu wamewekwa chini ya ulinzi katika kituo cha polisi cha Kilimani.

Mwili unasubiri kufanyiwa upasuaji katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Coptic.

View Comments