LSK imemtaka Koome kulinda Uhuru wa idara ya mahakama
Chama cha mawakili nchini LSK kimemtaka jaji mkuu Martha Koome kulinda uhuru wa idara ya mahakama.
Chama hicho kinasema jaji huyo anachukua usukani wakati ambapo kuna ongezeko la uvamizi dhidi ya maafisa wa mahakama na watu ambao hawajaridhika na maagizo ya korti. Aidha, Mkurugenzi mkuu Mercy Wambua amemhakikishia Koome kwamba kama mawakili watamuunga mkono bara-bara.
Hafla ya kuapishwa kama Jaji mkuu Koome iliandaliwa siku ya Ijumaa katika ikulu ya rais mjini Nairobi na kuongozwa na rais Uhuru Kenyatta na kuendeshwa na msajili mkuu wa idara ya mahakama Anne Amadi.
Koome anasema kiapo ambacho alilishwa kitamkumbusha kila wakati nguvu ambazo amepewa kuwahudumia wakenya na kuhakikisha kwamba haki inatolewa bila woga wala ubaguzi.
Ameitaka serikali kuhakikisha idara ya mahakama inapata mgao wa kutosha wa raslimali na vile vile maagizo ya mahakama yanafuatwa.