In Summary

•"Alionekana kutomtambua mwanaume yule aliyekuwa amevaa kofia na barakoa. Alisimama na kujitambulisha kuwa ni yeye Celestine. Mwanaume huyo akamwambia ‘ulidhani sitakupata. Unanicheza’ kisha kutoa kisu mfukoni na kuanza kumdunga bila huruma” mwenzake aliyeshuhudia tukio lote alisema.

Celestine Muthengei
Image: Hisani

Wanafunzi katika chuo kikuu cha Mt Kenya mjini Thika wanalia kilio cha haki baada ya mmoja wao kudungwa kwa  kisu hadi kufa na mwanaume aliyedai kuwa mpenzi wake.

Celestine Muthengei, 19, ambaye hadi mauti yake  alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili.alitendewa unyama huo kwenye chumba chake mbele ya wenzake wanne siku Jumatatu mida ya saa mbili usiku.

Kabla ya kumuua, mwanaume huyo anadaiwa kusema kuwa marehemu alikuwa anamcheza kisha kutoa kisu na kumdunga mara kadhaa kwenye sehemu mbali mbali mwilini na kuondoka.

Ripoti ya polisi iliashiria kuwa marehemu alifariki punde baada ya kufikishwa kwenye hospitali ya Thika Level 5 kutokana na majeraha ya kisu kwenye kifua, mgongo, kichwa na mbavu.

Marafiki waliokuwa wanaishi na Muthengei walisimulia kuwa muuaji huyo aliyejitambulisha kama mpenzi wake aliingia chumbani chao punde baada yao kumaliza chajio na kuulizia alipokuwa Muthengei.

Aliingia na kuuliza kwa upole alipokuwa Celestine. Alikuwa mpole sana hakuna ambaye angeshuku kuwa alikuwa na nia mbaya. Tulifikiria kuwa alikuwa mwanafunzi mwenzake aliyetaka usaidizi” mmoja wao alisema.

Inadaiwa kuwa kwa wakati ule, Muthengei alikuwa amekalia kitanda moja karibu na mlango huku akitia simu yake moto.

Alionekana kutomtambua mwanaume yule aliyekuwa amevaa kofia na barakoa. Alisimama na kujitambulisha kuwa ni yeye Celestine. Mwanaume huyo akamwambia ‘ulidhani sitakupata. Unanicheza’ kisha kutoa kisu mfukoni na kuanza kumdunga bila huruma” mwenzake aliyeshuhudia tukio lote alisema.

Baada ya tukio hilo la kuogofya, wasichana wale wanne walianza kupiga mayowe na kuomba usaidizi ila hakuna aliyesikia kilio chao kwani mhalifu yule alikuwa amefunga mlango upande ya ndani.

Muuaji yule aliondoka baada ya kuona Muthengei akiwa anavunja damu vibaya.

“Alipogundua kuwa Celestine anavunja damu vibaya, alifungua mlango na kutoweka kwenye giza” mwenzake alisimulia.

Wenzake walisisitiza kuwa walimjua mpenzi wa marehemu ila aliyetekeleza kitendo kile si yeye.

Punde baada ya mshukiwa kuondoka, wasichana wale walimchukua Muthengei na kumkimbiza hospitalini ila akakata roho alipofika. Waliendelea kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha Thika.

Maafisa wa polisi wangali wanamuwinda mshukiwa ambaye hajulikani aliko.

Wenzake marehemu walimtaja kuwa mnyenyekevu, mkarimu na alikuwa makini kwenye masomo yake.

Wakuu wa chuo cha MKU wameapa kuwapa ushauri wa kisaikologia wanafunzi walioshuhudia kitendo hicho cha unyama.

View Comments