In Summary

•Watoto waliokuwa wanaelekea shuleni waliona gunia lenye damu lilikokuwa limeachwa kando ya barabara moja mjini humo na kufahamisha watu ambao waliita polisi.

Mwanamume akichunga ng'ombe katika kituo cha polisi cha Awendo ambacho kilikamilika miaka mitano iliyopita, lakini mgogoro wa ardhi mahakamani umezuia matumizi yake.
Image: MANUEL ODENY

Polisi katika kaunti ya Migori wameanzisha uchunguzi baada ya mwili wa mwanamke usio na kichwa kupatikana ukiwa umetupwa mjini Awendo asubuhi ya Ijumaa.

Watoto waliokuwa wanaelekea shuleni waliona gunia lenye damu lilikokuwa limeachwa kando ya barabara moja mjini humo na kufahamisha watu ambao waliita polisi.

Bosi wa polisi katika kaunti ndogo ya Suna Mashariki Esau Ochorokodi alisema walipokea ripoti ya kwanza mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

"Kiongozi wa jamii aliwafahamisha polisi ambao walifika katika eneo la tukio na kukuta mwili wa mwanamke mzima ukiwa umewekwa kwenye gunia. Haukuwa na kichwa,” Ochorokodi alisema

Ochorokodi alisema mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya hospitali ya rufaa ya Migori ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti. Alisema  polisi wameanzisha uchunguzi  kubaini wahalifu waliotekeleza unyama huo.

"“Tunatoa wito kwa umma kusaidia polisi katika uchunguzi kwa kutoa taarifa za washukiwa. Tumeongeza doria na mikusanyiko wa kijasusi,” Ochorokodi alisema.

Tukio hilo limewashinikiza wakazi kutoa wito zaidi kwa serikali kufungua kituo cha polisi katika eneo hilo.

Tangu mwanzo wa mwaka huu, wakazi wa mji wa Awendo wamekuwa wakikabiliana na ukosefu wa usalama.

Mapema mwezi huo, mlinzi mmoja alikatwakatwa hadi kifo huku mwalimu wa Shule ya Msingi ya Manyatta akinusurika kifo baada ya kiganja chake cha mkono wa kushoto kukatwakatwa na washambuliaji.

View Comments