In Summary

•Mwanasiasa huyo amejitolea kumsaidia Bi Wangui Wambeca kupata haki kufuatia kifo cha mtoto wake siku ya Jumamosi.

•Sonko ameshauri vijakazi kutotumia watoto wasio na hatia kama zana ya kulipiza kisasi dhidi ya wadosi wao.

Mike Sonko ajitolea kumsaidia mama wa mtoto aliyepigwa hadi kufa na kijakazi
Image: HISANI// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ameomba kusaidiwa kumpata mama ya mtoto anayeripotiwa kupigwana kijakazi vibaya hadi kufariki.

Mwanasiasa huyo amejitolea kumsaidia Bi Wangui Wambeca kupata haki kufuatia kifo cha mtoto wake siku ya Jumamosi.

"Wafuasi wangu wamekuwa wakinitumia kisa hiki cha mtoto aliyevamiwa na msaidizi wa nyumba na kufariki siku 3 baadaye kutokana na kuvuja damu kwa ndani na matatizo. Yeyote aliye karibu na huyo mama amwambie awasiliane nami kwa ajili ya haki," Sonko ametangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Kijakazi anayetambulishwa kama Maureen Nyaboke anadaiwa  kumchapa mtoto huyo vibaya Jumanne wiki iliyopita kabla ya kupigwa kalamu siku iliyofuata.

Mtoto huyo anaripotiwa kufariki siku ya Jumamosi kutokana na matatizo yaliyosababishwa na  majeraha ya ndani.

Mshukiwa anadaiwa kuingia mitini tangu alipofutwa kazi baada ya kutekeleza unyama huo na msako mkubwa wa kumpata umeanzishwa.

Sonko ameshauri vijakazi kutotumia watoto wasio na hatia kama zana ya kulipiza kisasi dhidi ya wadosi wao.

"Alafu vijakazi mkiwa na mizozo na mdosi wako bonga na yeye mtafute suluhu. Usiwadhuru watoto wadogo  wasio na hatia kama huyu mzuri kwa sababu ya kulipiza kisasi," Sonko aliandika.

Wanamitandao wengi wamelaani kisa hicho na kutaka mshukiwa atiwe mbaroni ili kujibu maswali kuhusiana na kifo cha mtoto huyo.

View Comments