In Summary

•Mhudumu wa bodaboda na abiria wake mmoja nwalipoteza maisha yao baada ya gari hilo  kupoteza mwelekeo na kugonga pikipiki yao.

•Gavana Kinyajui alisema watu wengine wawili walionusurika kwenye ajali hiyo wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja ya Nakuru.

Gari la kampeni la gavana Kinyajui lililohusika kwenye ajali
Image: JAMES MUNYUA

Watu wawili walifariki katika ajali ya barabarani iliyohusisha gari la kampeni la gavana wa Nakuru Lee Kinyajui na bodaboda.

Mhudumu wa bodaboda na abiria wake mmoja ndio waliopoteza maisha baada ya gari hilo lililokuwa likiendeshwa na dereva wa kike kupoteza mwelekeo na kugonga pikipiki yao katika eneo la Free Area kwenye barabara Nairobi-Nakuru.

Gavana Kinyajui kupitia taarifa alisema ajali hiyo ilitokea Jumatatu mwendo wa saa tano asubuhi huku akifariji familia za waliopoteza maisha yao. Alisema watu wengine wawili walionusurika kwenye ajali hiyo wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja ya Nakuru.

"Tunasikitika kutangaza kuwa watu wawili walipoteza maisha huku wawili walionusurika wakiendelea kupokea matibabu. Rambirambi zetu za dhati kwa familia za marehemu. Wakati huo huo, tunahakikisha kwamba waathirika wote wanapewa huduma ya matibabu inayostahili," Kinyajui alisema  kupitia Facebook.

Gavana huyo wa muhula wa kwanza pia alitumia fursa hiyo kuhamasisha watu kuhusu usalama wa barabarani na kuwaagiza madereva kumakinika zaidi.

Kinyajui ambaye alichaguliwa kama gavana wa Nakuru katika chaguzi za 2017 anatetea wadhifa wake kwa tikiti ya Jubilee.

Ni mmoja wa wanasiasa kumi na wawili ambao walihojiwa na jopo la kuteua mgombea mwenza wa muungano wa Azimio mapema mwezi huu.

Kinyajui ni miongoni mwa wandani wa rais Kenyatta ambao wameendelea kuwa waaminifu kwa serikali yake katika muhula huu wake wa mwisho.

View Comments