In Summary

•Isaac Wafula Bukhebi, 47, Mkuu wa shule ya sekondari ya Bosto, aliripotiwa kutoweka Alhamisi jioni, Septemba 8.

•Mkuu wa polisi alifichua kuwa mwili wa marehemu ulipatikana katika Mto Nzoia.

Marehemu Isaac Bukhebi , mkuu wa shule ya upili ya Bosto ambaye mwili wake ulitolewa kutoka mto Nzoia
Image: DAVID MUSUNDI

Mwalimu mkuu wa shule moja ya upili katika kaunti ya Bomet alipatikana amefariki katika mto Nzoia katika eneo la Brigedia mpakani mwa Kaunti za Bungoma na Trans Nzoia.

Isaac Wafula Bukhebi, 47, Mkuu wa shule ya sekondari ya Bosto, aliripotiwa kutoweka Alhamisi jioni, Septemba 8.

Alikuwa amemjulisha mke wake kwamba ameenda kununua mjazo wa simu katika soko la Makhele iliyo Kapkoi karibu na Moisbridge ambako familia yake inaishi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kiminini John Onditi alithibitisha kisa hicho.

Alisema mke wa marehemu aliripoti tukio la kutoweka kwa mumewe mnamo Jumanne, Septemba 13.

Mkuu wa polisi alifichua kuwa mwili wa marehemu ulipatikana katika Mto Nzoia.

Mwili huo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kitale.

Mkuu wa polisi alifichua kuwa ripoti ya uchunguzi wa maiti ilionyesha kuwa mfumo wa mwili wa marehemu ulidokeza kwamba alikuwa amekula chakula chenye sumu.

“Kuwepo kwa sumu kwenye chakula kunadhihirisha wazi kuwa marehemu angeweza kuwekewa sumu au kujiwekea sumu, alama kwenye mwili wake zinaweza pia kuwa ni matokeo ya kugongwa na mawe mtoni,” alisema.

Viongozi wa Trans Nzoia wakiongozwa na gavana George Natembeya walisikitishwa na kifo cha mwalimu huyo mkuu.

"Hili ni tukio la kusikitisha sana kutokea. Nimesikitishwa sana na kifo cha mkuu wa shule. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi," alisema Natembeya.

Mwakilishi wadi mteule wa Wadi ya Waitaluk, Lusweti Furaha, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kuppet Kaunti ya Trans Nzoia, aliwapa rambi rambi familia na marafiki wa marehemu mwalimu mkuu, akisema kwamba udugu wa walimu umempoteza mtu wa kuheshimika.

Marehemu Bw Bushebi aliwahi kuwa naibu mkuu wa shule ya sekondari Friends Bwake Boys iliyoko Cherangany kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Shule ya Friends Masaba.

Baadaye alihamishiwa shule ya upili ya Toro Mainek na baadaye shule ya sekondari ya Bosto iliyoko Bomet ambako alihudumu hadi kufa kwake.

View Comments