logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Buriani! Watoto 5 wa wanandoa wa Nakuru wazikwa kwenye jeneza moja

Miili yao yote iliwekwa kwenye jeneza moja na kuzikwa pamoja.

image
na Radio Jambo

Makala04 February 2023 - 05:36

Muhtasari


•Watoto hao walizikwa Ijumaa nyumbani kwa wazazi wao katika eneo la Bahati, Kaunti ya Nakuru.

•Baba yao, Simon Ndung'u hata hivyo alihudhuria na kuwaongoza waombolezaji katika ibada hiyo. 

wazikwa katika jeneza moja nyumbani kwa wazazi wao Bahati.

Watoto watano wachanga wa dereva wa Nakuru Simon Ndung'u Kinyajui ,28, na mke wake Margaret Wangui ,25, ambao waliaga dunia masaa machache tu baaada ya kuzaliwa hatimaye wamezikwa.

Watano hao ambao walifariki katika hospitali ya Nakuru Level Five siku ya Jumatano walizikwa Ijumaa nyumbani kwa wazazi wao katika eneo la Bahati, Kaunti ya Nakuru. Miili yao yote iliwekwa kwenye jeneza moja na kuzikwa pamoja.

Mama ya watoto hao, Margaret Wangui, hata hivyo hakuhudhuria hafla ya mazishi kwani bado alikuwa amelazwa hospitalini.

Baba yao, Simon Ndung'u hata hivyo alihudhuria na kuwaongoza waombolezaji katika ibada hiyo. Wanachama wa 2NK Sacco, ambao wanafanya kazi pamoja na Ndung'u pia walikuwepo kumfariji mwenzao.

Mbunge wa eneo la Bahati, Irene Njoki, pia alituma wawakilishi kutoka ofisi yake kumwakilisha katika hafla hiyo.

"Naitakia familia amani, faraja, ujasiri na upendo mwingi wakati huu wa huzuni. Ofisi yangu itawasaidia wazazi na familia katika kipindi hiki kigumu," Mhe Irene alisema siku ya Ijumaa.

Siku ya Alhamisi, Afisa Msimamizi wa Matibabu wa Hospitali ya Nakuru Level 5, Aisha Maina alisema Margaret Wairimu mwenye umri wa miaka 25 alijiwasilisha katika kituo hicho akiwa mjamzito mnamo Januari 29.

"Alikuja kupitia eneo la  wagonjwa wa nje wa hospitali akiwa hana raha na walipomchunguza, madaktari waligundua kuwa alikuwa na mimba ya watoto wengi," Maina alisema.

Maina alisema mwanadada huyo alilazwa kwa uangalizi kwa sababu alikuwa na ujauzito uliozingirwa na hatari.

Alisema maumivu hayo yalizidi, na kuwalazimu madaktari kufanya upasuaji wa dharura ili kuwaokoa mama na watoto.

"Watoto hao walizaliwa wakiwa na miezi sita na ilibidi wawekwe kwenye incubator ili waweze kuishi," alisema.

Maina alisema watoto hao, wasichana wanne na mvulana mmoja walikuwa na uzito wa kati ya gramu 500 na 650 walipozaliwa.

Wanandoa hao wenye umri wa makamo wana mtoto mwingine wa miaka 4.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved