In Summary

•Raila Odinga ameishutumu serikali ya Rais William Ruto kwa kukatiza juhudi za upatanishi za Rais wa Tanzania Samia Suluhu nchini humo.

•Katika harakati zake za kuleta mageuzi, Raila ameapa kutumia njia za kisheria na za kiraia ili kuhakikisha mahitaji ya nchi yanatimizwa.

Image: BBC

Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga ameishutumu serikali ya Rais William Ruto kwa kukatiza juhudi za upatanishi za Rais wa Tanzania Samia Suluhu nchini humo.

Rais Ruto ametofautiana na mshirika wake wa zamani, Raila kuhusu ongezeko la ushuru na gharama ya juu ya maisha.

Katika kikao na vyombo vya habari vya Kimataifa leo Jumanne, Raila alifichua kuwa Rais Suluhu alizuru Kenya majuma mawili yaliyopita lakini hakuna mawasiliano ambayo serikali ilifanya naye kuhusu jitihada za kuwaleta Pamoja rais Ruto na Odinga.

Chanzo cha uhakika kutoka serikali ya Tanzania ambacho hakikutaka kutajwa jina lake kimeithibitishia BBC Swahili kuwa madai ya Raila yana ukweli.

“Rais wa Tanzania [Samia Suluhu] alikuwa nchini (Kenya)wiki mbili zilizopita. Ilikuwa ni kwa mwaliko wa [Rais] Ruto. Alibaki akisubiri. Tulikuwa tayari, lakini wao [Kenya Kwanza] hawakupatikana. Kwa kweli, ilimbidi kukaa huku kwa mbili,” Raila aliambia wanahabari.

Ili kukabiliana na athari za maandamano ya kuipinga serikali ambayo yaligeuka kusababisha maafa na kujeruhiwa kwa wafuasi wake, Raila anasema Muungano wa Azimio utaanzisha msukumo wa kukusanya pesa zinazolenga kuzisaidia familia za waliofariki na waandamanaji waliojeruhiwa.

"Kwa familia ambazo zimepoteza wapendwa wao, tunawapa pole na kuwaombea waliojeruhiwa hospitalini. Ndio maana tulisitisha maandamano ya kesho, ili kuomboleza. Pia tutazindua mpango wa fedha kusaidia familia za walioachwa na waliojeruhiwa.’ Odinga aliongeza .

'Kodi zaidi ni mzigo kwa Wakenya'

Katika mazungumzo yake na wanahabari hao kutoka mashirika ya kimataifa ya vyombo vya habari, Raila ameshikilia msimamo wake wa kutaka serikali shirikishi, heshima kwa vyama vyote vya kisiasa, mageuzi ya Tume ya Uchaguzi-IEBC, kubatilisha Sheria ya Fedha, 2023, na kupunguza gharama ya maisha.

“Huwezi kukabiliana na gharama ya juu ya maisha kwa kuongeza kodi. Wanasema kwamba [kodi] itatumika kulipa deni. Ikiwa uchumi umedorora ulimwenguni kote, unaongeza pesa kwenye uchumi.

Walichofanya ni kuendelea kuchimba shimo zaidi. Kwa nini nasema hivi? Ni kwa sababu tumewahi kufika hapa awali na [marehemu] Rais Kibaki na tukajiondoa.”

Katika harakati zake za kuleta mageuzi, Raila ameapa kutumia njia za kisheria na za kiraia ili kuhakikisha mahitaji ya nchi yanatimizwa.

Anasema kuwa hawezi kuchukua njia ya kisheria peke yake, kwa sababu serikali ina historia ya kutotii amri za mahakama.

"Lazima iwe mchanganyiko wa njia za mahakama na za kiraia. Hii ni kwa sababu hawaheshimu maamuzi ya mahakama.

Kwa mfano, mahakama ilisitisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha, 2023, inayoongeza VAT(Tozo ya thamani ya bidhaa) kwenye mafuta kutoka asilimia 8 hadi 16. Tume ya kawi imepuuza na kuitekeleza.

Ndiyo maana inatubidi tupiganekwa ncha mbili- mitaani huku tukiendelea kupigana mahakamani.”

View Comments