In Summary

•Suala hilo limeifanya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwaita tena wajumbe wake kutoka Kenya na Tanzania ambayo ni mwenyeji wa makao makuu ya EAC.

•Kufuatia mzozo wa hivi punde, uhusiano wa DR Congo na Kenya unaonekana kuzorota zaidi, huku Kenya ikishutumiwa kuwa mwenyeji wa "muungano haribifu".

Rais wa Kenya William Ruto (kushoto) alikuwa Kinshasa kukutana na mwenzake wa Kongo Felix Tshisekedi (Kulia) mwezi Novemba mwaka jana.
Image: BBC

Kuzinduliwa kwa muungano wa waasi wa Kongo katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kumetatiza uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya.

Hatua hiyo pia imezidi kuzorotesha uhusiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na jumuiya ya kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo ni mwanachama wake hivi karibuni.

Suala hilo limeifanya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwaita tena wajumbe wake kutoka Kenya na Tanzania ambayo ni mwenyeji wa makao makuu ya EAC.

DR Congo pia imewazuia waangalizi wa EAC kuingia nchini humo kufuatilia uchaguzi utakaofanyika Jumatano.

Mzozo unahusu nini?

Mwishoni mwa wiki, ,mkuu wa zamani wa baraza la uchaguzi la DR Congo, Corneille Nangaa alitangaza katika hoteli moja ya Nairobi kwamba anaunda muungano wa kisiasa, kijeshi na waasi wa M23 na makundi mengine yenye silaha ili kurejesha amani.

Alikuwa na Bertrand Bisimwa, mkuu wa M23, mojawapo ya makundi makubwa zaidi ya waasi ambayo yamekuwa yakiendesha harakati zake mashariki mwa DR Congo. Kuna tuhuma kwamba M23 inaungwa mkono na Rwanda, jambo ambalo Rwanda imekuwa ikikanusha.

Bw Nangaa hapo awali alitilia shaka uhalali wa urais wa Felix Tshisekedi nchini DR Congo. Na ukweli kwamba tangazo la muungano wake na M23 lilifanywa nchini Kenya lilivutia hisia kali kutoka Kinshasa.

Iliitaka Kenya kukomesha harakati za waasi katika ardhi yake.

Jibu la Kenya lilikuwa nini?

Siku ya Jumapili, Rais wa Kenya William Ruto aliwaambia waandishi wa kwamba alikataa kutii ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo la kuwakamata wanasiasa hao kwani lingekuwa "sio la kidemokrasia".

"Kenya ni nchi ya demokrasia. Hatuwezi kumkamata mtu yeyote ambaye ametoa tamko. Hatuzuii watu kwa kutoa matamshi, tunakamata wahalifu," alisema.

Wizara ya mambo ya nje ya Kenya hapo awali ilisema "inajitenga vikali" na masuala ya ndani ya DR Congo, na kuongeza kuwa imeanza kuchunguza suala hilo.

"Kenya inathibitisha zaidi kutojihusisha na masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na inaunga mkono amani, usalama na uimarishaji wa kidemokrasia wa nchi," ilisema.

Kujitokeza nchini Kenya kwa kiongozi wa M23 na Bw Nangaa, ambaye sasa anaishi uhamishoni, kuliiangazia serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo "kwa njia mbaya sana", mchambuzi wa sera za kigeni aliambia BBC.

Macharia Munene, profesa wa historia na uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani nchini Kenya, alisema serikali ya Kongo ni wazi haikufurahishwa na tukio hilo.

Inamaanisha nini kwa uhusiano wa kikanda?

Kufuatia mzozo wa hivi punde, uhusiano wa DR Congo na Kenya unaonekana kuzorota zaidi, huku Kenya ikishutumiwa kuwa mwenyeji wa "muungano haribifu".

"Nilitaka kuwakumbusha [Kenya] kuzingatia sheria na inayotuunganisha shasa katiba ya jumuiya ya mataifa ya Afrika Mashariki, ambayo inahakikisha kwamba hatuwezi kushambuliana sisi kwa sisi, kwamba hatuwezi kudumisha makundi yenye silaha ambayo yanavuruga uhusiano wa nchi zetu," Waziri wa Mambo ya Ndani wa DR Congo Peter Kazadi alisema katika taarifa.

Kenya na DR Congo zimefurahia uhusiano mzuri wa kidiplomasia hapo awali.

Kenya imekuwa mwenyeji wa mazungumzo kadhaa na wawakilishi wa makundi makubwa ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mwaka uliopita katika harakati za kutafuta amani katika eneo hilo. Mazungumzo hayo yamekwama.

Aidha, wanajeshi wa Kenya walikuwa sehemu ya kikosi cha Afrika Mashariki kilichoundwa ili kukabiliana na ghasia za wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Image: BBC

Vikosi hivyo viliamriwa kuondoka nchini mapema mwezi huu kufuatia wasiwasi wa serikali ya Kinshasa kwamba havifanyi kazi.

DR Congo ilijiunga na EAC mwaka jana, lakini uanachama wake umekuwa mgumu kutokana na hisia kwamba Bw Tshisekedi, pamoja na wataalam wa Umoja wa Mataifa, wanasema mwanachama mwenzake Rwanda anaunga mkono M23, jambo ambalo Rwanda inakanusha.

Je, utawala mpya wa Kenya umebadilisha mahusiano?

Rais Ruto aliyeingia madarakani mwaka jana anaonekana kuwa na mtazamo tofauti na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

Bw Kenyatta alikuwa rafiki wa karibu na Bw Tshisekedi na alisemekana kwa alichangia pakubwa kushinikiza DR Congo kujiunga na EAC.

Inasemekana alikuwa rais pekee wa taifa la Afrika kuhudhuria kuapishwa kwa Bw Tshisekedi mnamo 2019 - huku kukiwa na kutoridhishwa na jumuiya ya kimataifa kuhusu matokeo ya uchaguzi.

Lakini Bw Ruto na Bw Tshisekedi wanasemekana kutokuwa na ukuruba.

Prof Munene anasema kuzorota kwa mambo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya kunaweza pia kuakisi uhusiano usiokuwa mzuri kati ya Bw Ruto na Bw Kenyatta.

"Tuna hali ambayo Bw. Ruto hana furaha na mtangulizi wake. Pengine ni hiyo hali ya kutokuwa na furaha na mtangulizi wake inajitokeza sasa dhahiri... Hii inawezekana ni dhihirisho la hali hiyo" anasema.

Huku Bw Ruto akitetea hatua ya Kenya kukataa kuwakamata viongozi wa waasi wa DR Congo, Bw Kenyatta amelaani muungano huo kama jaribio la kupinga "hali halisi ya kisiasa iliyopo [DR Congo]".

Taarifa ya ofisi yake ilisema "sikubaliani na muungano huo hasa mwenendo wao wa kijeshi, na matamshi yanayolewa katika mazingira ya kisiasa iliyopo kwa sasa ni uchochezi".

Bw Kenyatta amekuwa mwezeshaji wa Mchakato wa Amani wa Nairobi unaoongozwa na EAC, akijaribu kufanikisha makubaliano ya amani kati ya DR Congo na waasi.

Ametoa wito wa kurefushwa kwa muda usiojulikana usitishaji vita ulioratibiwa na Marekani hivi karibuni katika eneo hilo ambao utaweka mazingira ya kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya amani.

Kipi kitakachofuata

DR Congo imetangaza kutakuwa na "athari" kwa Kenya kuwakaribisha viongozi wa waasi wa Kongo katika ardhi yake.

Na kwa mara ya kwanza tangu EAC iundwe, imezuiwa kufuatilia uchaguzi katika nchi wanachama.

Prof Munene anasema Kenya inafaa kusuluhisha mzozo huo wa kidiplomasia "kwa uangalifu na bila kukurupuka".

Anasema wakati muungano wa waasi hauwezi kuleta tishio la mara moja kwa mamlaka ya Kongo, hilo linaweza kubadilika kwa wakati ufaao.

View Comments