In Summary

•Alisema kuwa kabla ya kocha huyo kutoka Rwanda kufariki, alikuwa katika hali ya furaha kwani binti yao alikuwa karibu kujiunga na shule.

•Alizungumza kuhusu uhusiano wa karibu ambao mumewe alikuwa nao na Kiptum akifichua kuwa alikuwa na mipango mikubwa kwake.

Bi Joan Chelimo alimuomboleza mumewe kihisia
Image: HISANI

Mke wa kocha wa mwanariadha aliyeaga Kelvin Kiptum, marehemu Gervais Hakizamana, Bi Joan Chelimo amemuomboleza kihisia mumewe huyo kutoka Rwanda.

Wakati alipokuwa akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano, Bi Chelimo alifichua kwamba mumewe alizungumza naye kupitia simu mara kadhaa siku aliyofariki, ikiwemoa dakika chache kabla ya kuhusika katika ajali iliyochukua maisha yake.

Alisema kuwa kabla ya kocha huyo kutoka Rwanda kufariki, alikuwa katika hali ya furaha kwani binti yao alikuwa karibu kujiunga na shule.

“Binti yetu anauliza baba yake yuko wapi. (Hakizamana) alikuwa karibu sana na binti yake, karibu sana,” Bi Chelimo alisema

Alifichua kwamba mwanariadha huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 37 alikuwa na mipango mikubwa sana kwa familia yao kwani alikusudia kuwahamisha hadi nchini Ufaransa ambako pia ana nyumba.

"Tulitakiwa kwenda Ufaransa mwaka jana. Sasa juu ya Kiptum akaniambia tungoje kidogo amshughulikie kwanza. Hapo tukaamua mtoto asome kwanza wakati akishughulikia Kiptum,” alisema.

Chelimo alisema siku ambayo mumewe alifariki, alimpigia simu kumtaarifu kuwa yuko njiani kuelekea nyumbani na angefika baada ya dakika 20. Mnyarwanda huyo hata hivyo hakufika nyumbani kwa dakika zile 20 alizoahidi.

Pia alizungumza kuhusu uhusiano wa karibu ambao mumewe alikuwa nao na Kiptum akifichua kuwa alikuwa na mipango mikubwa kwa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon.

"Aliniambia hivi majuzi kwamba wanataka kuvunja rekodi ya chini ya saa mbili," alisema.

Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, sasa ameomba usaidizi ili kukabiliana na kifo cha mwanamume aliyekuwa akimsaidia yeye na familia yake.

Kiptum atazikwa Jumamosi, Februari 24. Familia ya Hakizamana iliyo nchini Rwanda bado haijatoa tarehe ya kuzikwa kwake.

View Comments