In Summary

•Bei ya kukodisha ndege ya kibinafsi ya kifahari ambayo yeye na ujumbe wake walisafiria inakadiriwa kuwa (Sh199.2m).

•Serikali ya Marekani ilikanusha ripoti kwamba ililipia ndege iliyotumiwa na Bw Ruto na ujumbe wake.

Image: BBC

Serikali ya Kenya imetetea gharama ya safari ya Rais William Ruto nchini Marekani.

Bei ya kukodisha ndege ya kibinafsi ya kifahari ambayo yeye na ujumbe wake walisafiria inakadiriwa kuwa (Sh199.2m) $1.5m (£1.2m), kulingana na kituo cha kibinafsi cha runinga cha KTN.

"Faida za ziara hii ni kubwa kuliko mara milioni kama hizo," msemaji wa serikali Isaac Mwaura aliambia BBC, bila kuthibitisha gharama.

Zaidi ya watu 30 akiwemo mcheshi maarufu wanaripotiwa kuandamana na rais huyo aliyetua Atlanta, Georgia siku ya Jumatatu.

Bw Ruto yuko katika ziara ya siku nne kwa mwaliko wa mwenzake wa Marekani Joe Biden. Ni ziara ya kwanza ya kitaifa kwa rais wa Kenya nchini Marekani katika miongo miwili na ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Afrika katika kipindi cha miaka 16.

Anatazamiwa kufanya mazungumzo na Bw Biden siku ya Alhamisi, yakiangazia ushirikiano wa kibiashara na usalama, ikiwa ni pamoja na ahadi ya Kenya kuongoza ujumbe wa mataifa mbalimbali kurejesha utulivu nchini Haiti.

Lakini baadhi ya Wakenya wameeleza kughadhabishwa na kukodi ndege kutoka kampuni ya RoyalJet inayomilikiwa na Dubai kwa ajili ya safari hiyo badala ya kutumia ndege yake ya kawaida ya rais ikizingatiwa hatua za kubana matumizi ya serikali na kupanda kwa gharama ya maisha.

Haijabainika ni kwa nini rais alichagua ndege hiyo ya kibinafsi lakini kumekuwa na wasiwasi wa usalama kuhusu ndege ya kawaida ya rais, inayojulikana kama Harambee One, ambayo ilinunuliwa takriban miaka 30 iliyopita.

Serikali ya Marekani ilikanusha ripoti kwamba ililipia ndege iliyotumiwa na Bw Ruto na ujumbe wake.

"Ili tu kuwa wazi: Marekani haikulipia ndege ya Rais Ruto kwenda Marekani," msemaji wa ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, aliwaambia waandishi wa habari.

Haya yanajiri huku kukiwa na hasira kuhusu mipango ya serikali ya kutoza ushuru wa ziada, huku Bw Ruto akiwataka Wakenya kuishi kulingana na uwezo wao.

Gharama ya mkate, uhamishaji wa pesa kwa njia ya simu, muda wa maongezi na data inatazamiwa kupanda huku serikali ikitafuta kuongeza ushuru wa ziada wa $2.4bn katika mwaka wa fedha unaoanza Julai.

Wakosoaji wanasema ushuru huo unasaidia tu kufadhili ubadhirifu serikalini badala ya kuboresha huduma za umma.

View Comments