In Summary

•KRC ilifichua kwamba mwanamke huyo  alijifungua salama kwa usaidizi wa Daktari Indanyenyi Luseso na mhudumu Mary Nyiha ambao pia walikuwa ndani ya treni hiyo.

•KRC ilithibitisha kwamba mwanamke huyo na mtoto wake mchanga wako sawa na salama baada ya tukio hilo la kipekee.

Mwanamke mmoja alijifungua ndani ya treni ya SGR Jumatano, Juni 21 2023.
Image: TWITTER// KRC

Siku ya Jumatano, Juni 21, mwanamke mmoja alijifungua kwa mafanikio akiwa ndani ya treni ya Madaraka Express inayojulikana kama treni ya SGR.

Katika taarifa ya Jumatano jioni, Shirika la Reli la Kenya lilifichua kwamba mwanamke huyo ambaye jina lake halikutajwa alijifungua salama kwa usaidizi wa mhudumu wa afya, Daktari Indanyenyi Luseso na mhudumu wa abiria, Bi Mary Nyiha ambao pia walikuwa ndani ya treni hiyo.

Treni hiyo ilikuwa ikielekea mji wa pwani wa Mombasa kutoka Nairobi.

"Tunayo furaha kushiriki hadithi ya kufurahisha ya mama ambaye alikaribisha mtoto kwenye treni ya Madaraka Express ya kusafirisha Abiria hadi Mombasa," taarifa ya KRC ilisoma.

"Tulibarikiwa kuwa na Dkt. Indanyenyi Luseso ambaye alitoa huduma hiyo, akisaidiwa na mhudumu wetu wa Abiria, Bi. Mary Nyiha. Baadaye, alikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Mariakani kwa usaidizi zaidi wa matibabu," iliendelea.

KRC ilithibitisha kwamba mwanamke huyo na mtoto wake mchanga wako sawa na salama baada ya tukio hilo la kipekee.

"Mama na mtoto wote wako sawa. Tunamtakia heri,"

Shirika la reli pia lilishiriki picha za mama huyo mpya, daktari na mhudumu wa abiria akiwa wamemshika mtoto huyo mchanga huku tabasamu kubwa zikiwa zimeandikwa kwenye nyuso zao.

Abiria wengine wenye furaha tele waliokuwa kwenye kibanda kimoja na mama huyo walionekana wakitazama kwa udadisi wakiwa mbali.

View Comments