In Summary

• Waziri Matinag'i alisema baada ya janga la Corona, Kenya sasa inapigana na janga lingine la wanasiasa wanaoropokwa na maneno bila mipango maalum.

Waziri wa usalama Fred Matiang'i na naibu rais William Ruto
Image: Facebook

Waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i amewakashfu baadhi ya viongozi wanaopinga mageuzi ambayo serikali inataka kutekeleza katika sekta ya bodaboda nchini.

Hii ni baada ya rais Kenyatta kutangaza sheria kali ili kudhibiti sekta ya bodaboda kufuatia tukio ambapo kundi moja la wahudumu wa boda boda walimdhulumu mwanamke.

Akizungumza katika kongamano la kitaifa la maboresho ya sekta ya bodaboda, Matiang’i alikosoa viongozi hao kwa kile kilichoonekana ni kumlenga moja kwa moja naibu wa rais William Ruto na wendani wake kwa kushambulia serikali  kuhusiana na oparesheni ya kulainisha sekta ya bodaboda.

Matinag’i alisisitiza kwamba serikali ina nia nzuri ya kuwarai wanabodaboda kujiunga na vyama vya ushirika (SACCOS)  na kwamba viongozi wanaopinga hawajui wanachokisema na kwa mara nyingi huwa wanaropokwa tu ili kutafuta kura.

“Acha niwambie, baada ya janga la Corona, sasa Kenya janga tunalolipiga vita ni janga la kuropokwa na maneno ya hila na propaganda. Unajua viongozi wa kisiasa ambao wanaamka tu asubuhi na kuanza kudanganya. Wanafanya ziara katika sehemu mbali mbali za nchi kudanganya tu. Baadhi yao mtu unaibika naos ana kwa sababu wanazungumza mambo ambayo hawajui. Viongozi hao hawajawahi shiriki katika maoni ya umma na wala hawana muda wa kuelewa maoni ya umma, hawajawahi kuwa na mazungumzo na watu wa maana, ndio maana wanaendelea tu kudanganya,” alisema dkt. Matiang’i.

Waziri huyo aliendeleza mikwara yake kwa kambi ya naibu rais William Ruto bila kumtaja mtu na kusema kwamba viongozi hao wanaopinga mageuzi ya maboresho katika sekta ya bodaboda kwa sababu wanataka kuambia wananchi mambo ya uongo ambayo wanapenda kusikia bila kuugeukia ukweli halisi wa mambo na kuyapanga inavyofaa.

“Wanasiasa hao wanachoma na kurubuni takwimu tu. Wanakuangalia tu na kuanza kukuambia, ooh nitakupatia bilioni 100, halafu wanakutana na kundi lingine wanasema, wewe nitakupatia bilioni 150, tena wanakutana na mwingine wanamwambia, wewe unaonekana vizuri nitakupa bilioni 200, yote haya bila mipango wala chochote bali maneno matupu,” Matiang’i alifoka.

View Comments