In Summary

• Bungei alisema walipokea maombi kutoka kwa vikundi viwili vilivyokuwa na nia ya kufanya maandamano siku moja na kuamua kutotoa kibali chochote cha kuandamana.

Mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei akihutubia wanahabari Jumapili, Machi 19, 2023.
Image: CYRUS OMBATI

Mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei ametangaza maandamano ya Azimio La Umoja One Kenya Alliance kuwa haramu.

Akihutubia wanahabari Jumapili, Bungei alisema maandamano hayo hayataruhusiwa kwa vile hayafikii kizingiti.

Kauli hiyo inafuatia mkutano wa makamanda wa polisi ulioitishwa Jumamosi na inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome katika ofisi zake katika jumba la Jogoo.

Kiini cha mkutano huo kilitajwa kuwa ni kutafuta mbinu mbadala za kuzima na kulemaza maandamano ya Odinga ambayo yanatarajiwa kuanza Jumatatu ya Machi 20 kote nchini, wakianzia jiji kuu la Kenya, Nairobi.

Mkutano huo ulikamilika kwa maelewano kwamba mkuu wa polisi kanda ya Nairobi Adamson Bungei angepewa maelekezo zaidi kabla ya kuhutubia wanahabari Jumapili.

Bungei alisema walipokea maombi kutoka kwa vikundi viwili vilivyokuwa na nia ya kufanya maandamano siku moja na kuamua kutotoa kibali chochote cha kuandamana.

Alisema jumuiya ya wafanyabiashara ya Azimio la Umoja na Nairobi iliwaandikia barua kuhusu nia yao ya kufanya maandamano siku ya Jumatatu.

“Mtu yeyote atakayevunja amani au kuvunja sheria wakati wa maandamano atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Hata hivyo, muungano wa upinzani ukiongozwa na Odinga umesisitiza kwamba maandamano yao yataendelea kama yalivyopangwa licha ya Bungei kusema kwamba hakuna kibali kilichotolewa kwa ajili ya maandamano hayo ambayo Azimio wanasisitiza yatakuwa ya amani na kuwataka wafanyibiashara wote kutokuwa na hofu ya kuharibiwa biashara zao.

Jumamosi, maafisa wa polisi pia waliwatia mbaroni wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya 50 ambao walikuwa na mkutano katika jumba la Chester na ambao ujumbe wao ulikuwa ni kuunga mkono maandamano hayo.

View Comments