In Summary

•Rais William Ruto amewasimamisha kazi kwa muda makamishna  wa IEBC wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera.

•Bunge la Kitaifa lilipiga kura Alhamisi usiku kupitisha ripoti ya kamati iliyopendekeza wanne hao waondolewe.

Makamishna wa IEBC Justus Nyangaya, makamu mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit na Francis Wanderi wakati wa mkutano uliopita na wanahabari katika hoteli ya Serena.
Image: REUTERS

Rais William Ruto amewasimamisha kazi kwa muda makamishna wanne wa IEBC waliotofautiana na mwenyekiti Wafula Chebukati kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera.

Katika notisi ya gazeti la rasmi la serikali iliyotolewa Ijumaa, Rais alisema wanne hao wataacha kazi  kwa muda mara moja.

Mbali na Cherera, makamishna wengine waliosimamishwa ni pamoja na Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irine Masit.

“Baada ya kupokea na kuzingatia ombi la Bunge na kutekeleza mamlaka aliyopewa kiongozi wa nchi na Serikali kwa mujibu wa Kifungu cha 251 cha Katiba, mimi, William Samoei Ruto, Rais na Amiri Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya. , naelekeza ifuatavyo: KWAMBA (1) Juliana Whonge Cherera, (2) Francis Mathenge Wanderi, (3) Irene Cherop Masit na (4) Justus Abonyo Nyang'aya, wakiwa wanachama wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, wamesimamishwa kazi mara moja," ilisema taarifa hiyo.

Bunge la Kitaifa lilipiga kura Alhamisi usiku kupitisha ripoti ya kamati iliyopendekeza wanne hao waondolewe.

Hii ni baada ya Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria kuthibitisha kwamba maombi manne yaliyokuwa yakitaka wanne hao kuondolewa yalifikia vigezo vya wao kutimuliwa afisini.

Rais pia alimteua Jaji wa Mahakama ya Juu Aggrey Muchelule kuwa mwenyekiti wa jopo maalum kuwachunguza makamishna hao wa IEBC.

Wengine walioteuliwa katika jopo hilo kama wanachama ni Carolyne Kamende Daudi, Linda Gakii Kiome, Mathew Njaramba Nyabena na Kanali (Mst.) Saeed Khamis Saeed.

Kibet Kirui Emmanuel, Irene Tunta Nchoe wameteuliwa kuwa makatibu.

Wakili mkuu wa jopo hilo ni Peter Munge Murage ambaye atasaidiwa na Zamzam Abdi Abib.

"Jukumu la jopo litakuwa kuzingatia ombi la kuondolewa kwa (1) Juliana Whonge Cherera, (2) Francis Mathenge Wanderi, (3) Irene Cherop Masit na (4) Justus Abonyo Nyang'aya kutoka ofisini kama makamishna. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kuchunguza madai hayo," Rais alisema.

View Comments